• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Siku ya Wanawake yaletea tabasamu wafungwa wanawake Thika

Siku ya Wanawake yaletea tabasamu wafungwa wanawake Thika

Na LAWRENCE ONGARO

WAFUNGWA wanawake  wa gereza la Thika walisherehekea Siku ya Wanawake Ulimwenguni kwa njia ya kipekee.

Wafungwa zaidi ya 100 walijumuika pamoja na jamaa zao mnamo Ijumaa katika jela ya Thika huku wakionyesha furaha nyusoni mwao.

Afisa mkuu wa kitengo cha wanawake, Bi MaryAnne Mutembei, alisema siku hiyo ilikuwa muhimu kwao kwa sababu waliweza kujumuika na jamaa zao, huku pia wakipata nafasi ya kujieleza waziwazi kwa umma jinsi wanavyokabiliana na maisha hapo gerezani.

Wahisani kadha walijitokeza kuwakabidhi vifaa muhimu vya matumizi.

Baadhi  ya mashirika yaliyojitolea kuwafaidi wafungwa hao ni B-Sound Entertainment and Partners, Rotary Club Thika, Mindset Trainers, Kenya National Library Services,  STC Women, na Equity Afya.

Vifaa vya matumizi vilitolewa kwa wafungwa wanawake wa Thika Prison na mashirika tofauti Machi 8, 2019. Picha/ Lawrence Ongaro

Wafungwa hao walinufaika na bidhaa mbalimbali zikiwa ni sabuni, dawa za kusugua meno, vipodozi vya kujipaka, vifaa vya watoto vya Pamppers na mahitaji mengine muhimu.

Bi Mutembei aliwapongeza wafadhili hao kwa kazi njema waliyofanya.

“Sisi kama idara ya gereza tunawapongeza wafadhili wote waliojitolea kuwafaa wafungwa wetu hapa Thika. Hii ni njia moja ya kuwapa motisha wafungwa hawa,” alisema Bi Mutembei.

Siku muhimu

Alisema siku hiyo ya wanawake ulimwenguni, ni muhimu kwa wafungwa kwa sababu wakipata nafasi ya kusherehekea na aila zao na pia kujieleza wazi kwa umma.

“Tuliweka siku hiyo kama yao ya kusherehekea na walipata nafasi ya kufanya upishi ambapo waliandaa pilau na nyama. Wakati huo pia walionyesha vipawa vyao vya uimbaji na maonyesho ya mitindo,” alisema Bi Mutembei.

Bi Carolyne Wanjiru, 30, aliyeshtakiwa kwa makosa ya uhalifu alisema kwa miezi sita sasa amejifunza mengi gerezani.

Alisema kwa sasa anafanya kozi ya ushonaji ambayo anatarajia itamsaidia atakapotoka gerezani.

“Ninawahimiza wanawake wenzangu walio kule nje wafuate sheria ili wasije kuvunja sheria na kujipata gerezani,” alisema Bi Wanjiru.

Baadhi ya wafungwa wachache wakipata nafasi ya kujieleza wazi bila wasiwasi.

Nao askari jela wanawake ‘walijiachilia’ kwa kuneng’ ua viuno bila wasiwasi huku muziki ukiendelea kunoga.

You can share this post!

Waasisi wa Handisheki

MWANAMKE MWELEDI: ‘Najionea fahari kuilinda...

adminleo