Simanzi gwiji wa ushairi akifariki
JUMA NAMLOLA na CHRIS ADUNGO
WAPENZI wa Kiswahili wamepata pigo baada ya mshairi mkongwe Abdalla Mwasimba kuaga dunia hapo Jumatano akiwa na umri wa miaka 83.
Jamaa na marafiki waliofika katika makaburi ya Waislamu ya Kariokor, Nairobi, walimmiminia sifa Mzee Mwasimba, ambaye ni Mkenya wa kwanza kuwahi kughani mashairi redioni.
Mtindo wake wa kughani ulivutia wengi, akiwemo mshairi Nuhu Zubeir Bakari almaarufu Al-Ustadh Pasua.
“Nimempoteza mwalimu aliyeniachia kikoba cha ughani wa mashairi. Alinichochea kuanza kuchangia mashairi magazetini nikiwa mwanafunzi wa darasa la sita. Ilikuwa tija kumsikiliza akighani tungo zangu redioni na imekuwa fahari kufanya naye kazi katika shirika moja,” akasema Bakari.
Mwasimba amekuwa akikagua na kusahihisha mashairi yanayochapishwa katika magazeti ya Taifa Leo na Taifa Jumapili. Aliugua kisukari na presha kwa muda mrefu.
Mwanawe mdogo wa kiume, Bw Mwasimba Abdallah, alisema babake alizidiwa na maradhi hayo Jumanne usiku na akakata roho mwendo wa saa kumi alfajiri.
Mtangazaji mkongwe Badi Muhsin alimsifia Mwasimba kuwa mwalimu wa wengi katika ushairi na tasnia ya uanahabari.
“Alikuwa mtu wa watu. Hakukosa ucheshi kila alipouliza maswali au kunasihi kupitia ushairi. Aliwahi kuniuliza: Iwapo mpera huzaa mapera, mwembe huzaa maembe, mgomba huzaa nini?”
Mashairi yake, Faida ya Pombe Nini, Mzungu Kutuita Bwana na Kuvaa Hirizi yaliwapa vijana changamoto ya kuachana na ulevi na kujitahidi kazini bila ya kutegemea mitishamba.
Kutokana na weledi wake katika ushairi, Mwasimba alitunukiwa tuzo kadhaa na Kituo cha Kiswahili cha WASTA kinachomilikiwa na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah mjini Ngong.
“Tumeondokewa na nguzo ya Ushairi wa Kiswahili na kigogo ambaye mashairi yake hayakuwa yakitungwa kwa kalamu. Alikirimiwa kipaji adhimu na uwezo wa kutunga papo kwa hapo.”
“Mwasimba alikuwa mnyenyekevu, mwenye roho safi na mwepesi wa kuitikia wito. Alihudhuria hafla zote za kutolewa kwa Tuzo za WASTA na akatufundisha umuhimu wa kuthamini Kiswahili,” akasema Guru Ustadh Wallah Bin Wallah.
Tuzo kubwa zaidi ambayo Mwasimba aliwahi kupata ni kutambuliwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2015.
Alipewa tuzo ya Head of State Commendation (HSC) kwa mchango wake katika makuzi ya Kiswahili.
Aliwahi pia kuongoza kikundi cha wanafunzi kutoka Nairobi, kughani shairi wakati wa sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Bara la Afrika mnamo 1987 katika uwanja wa MISC Kasarani.
Mwingine aliyewaongoza wakereketwa wa Kiswahili kumuomboleza Mwasimba ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Yearbook Editorial Board, Bw Edward Mwasi.
“Tumepoteza gwiji, malenga na mshairi hodari. Nilifanya kazi na Mwasimba katika gazeti la Taifa Leo nilikosimamia usanii wa michoro. Alikuwa mcheshi na Kiswahili kilimtiririka kwa urahisi kabisa. Alichangia sana makuzi ya lugha hii Afrika Mashariki. Kwa heri shujaa,” akasema Mwasi.
Mwanahabari wa Radio Maisha, Hassan Kauleni mwana wa Ali, alisema: “Kwake Mola ndiko tutokako na kwake ndiko turejeako. Kila nafsi itaonja mauti. Lala salama mzee wetu.”
Mwasimba alizaliwa mnamo 1937 katika eneo la Msambweni, Kaunti ya Kwale. Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msambweni na akaachia masomo katika darasa la tano. Mnamo 1955, alielekea Tanganyika kujifunza ulehemu (welding) katika Shule ya Ifunda, Mkoani Iringa.
Aliporejea Kenya mnamo 1956, alipata kibarua cha kuchomelea vyuma katika mojawapo ya karakana za kutengeneza vitanda na madirisha jijini Mombasa. Alihamia Nairobi mwishoni mwa 1957.
Umahiri wake wa kutunga na kuimba mashairi uliwaridhisha vinara wa Kenya Broadcasting Service (kabla ya kuitwa VOK) kiasi kwamba walimpa jukumu la kuyaghani mashairi katika kipindi kilichoongozwa na Hassan Mazoa, Daniel Katuga, Mahfudh Bawazir, John Nzau na baadaye Khadija Ali. Alihudumu huko kati ya 1958 na 2003 kisha akapata nafasi ya kuendesha kipindi ‘Dunia Ina Mambo’ katika runinga ya QTV .
Malumbano ya hoja nzito zenye busara kuhusu masuala ya ndoa na dini kati ya Pala Mlanzi Hassan kutoka Rufiji na Shabaan Bin Robert kutoka Tanga, Tanganyika yalimvutia sana tangu utotoni.
Kwa hofu ya kutoruhusu chochote kumfutu katika mijadala yao, ilimlazimu kila siku kusoma magazeti ya ‘Mamboleo’ (Tanganyika) na ‘Baraza’ (Kenya). Mashairi ya wawili hao yalichapishwa katika magazeti hayo.
Akiongozwa na tamaa ya kuvifikia viwango vyao, Mwasimba alimtungia msichana mmoja wa darasa la tatu shairi la mapenzi ambalo liliwasisimua walimu na wanafunzi wote shuleni Msambweni mnamo 1947. Hapo ndipo kipaji chake cha kutunga mashairi kilianza kudhihirika.
Wakati akiyaghani mashairi KBC, pia aliaminiwa kuendesha vipindi ‘Ubingwa wa Lugha’, ‘Kuzungumza ni Kuelewana’ na ‘Baraza la Wazee’.
Kwa kuwa uigizaji ni kipaji kilichojikuza ndani ya Mwasimba tangu akiwa tineja, alianza kutunga na kurekodi michezo ya kuigiza ya ‘Usipoziba Ufa’, ‘Mchezo wa Wiki’, ‘Ushikwapo Shikamana’ na ‘Kikulacho Ki Nguoni Mwako’.