Habari Mseto

Simanzi na majonzi Wangechi akizikwa

April 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

IRENE MUGO na NICHOLAS KOMU

MWANAFUNZI aliyeuawa wa Chuo Kikuu cha Moi Ivy Wangechi, alizikwa Alhamisi katika sherehe iliyokuwa na msisimko nyumbani kwa wazazi wake eneo la Mahiga, Nyeri.

Ilikuwa ni kilio na majonzi katika mazishi hayo eneo la Othaya gari lililobeba mwili wa Ivy lilipowasili nyumbani.

Mwanafunzi huyo wa miaka 25, inadaiwa kuwa aliuawa na rafikiye wa utotoni mnamo Aprili 9 katika eneo la Chuo Kikuu cha Rufaa na Mafunzo cha Moi, mjini Eldoret.

Familia na marafiki walisema alikuwa mwanafunzi mwenye kujitolea na mwenye furaha na kucheka sana, mrembo na mwerevu.

Kulingana na familia yake, alikuwa ni mtu wa kuigwa na binamu na nduguze na alikuwa tumaini la wazazi wake.

Alikuwa akipenda sana mambo ya fasheni na alikuwa na shoo katika Shule ya Wasichana ya Alliance na akiwa chuoni alikuwa mwigizaji wa maonyesho ya kimitindo.

Mamake, Bi Winfred King’ori, huku akiwa amevalia nguo ya kijani kibichi, alipiga unyende alipoona jeneza la bintiye huku jamaa wakimfariji.

Alisema hakujua hatua ambayo angechukua kwani maisha yake yaligeuka kuwa kiza kutokana na mauaji ya bintiye.

“Ni nani ataninunulia mikoba, herini na manukato? Nani atanirekebisha nikijwa kombo?

Dada na nduguye waliachwa tu na kumbukumbu za wakati walipokuwa pamoja, “Sikudhania ningekupoteza, bado sijaamini. Sijui nitachukua vipi majukumu yako ya mwana wa kwanza, sijui ikiwa niko tayari,” alisema dadake Cheryl Githui.

Viongozi waliozungumza walitaka sheria iimarishwe kudhibiti uchokozi mitandaoni.