• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Simu ya Uhuru ilitumika kwa ulaghai wa Sh10 milioni, mahakama yaambiwa

Simu ya Uhuru ilitumika kwa ulaghai wa Sh10 milioni, mahakama yaambiwa

Na Richard Munguti

KULIKUWA na makabiliano makali mahakamani jana kati ya wakili Cliff Ombeta na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (SADPP), Edwin Okello, baada ya wakili huyo kudai kuwa nambari ya simu ya Rais Uhuru Kenyatta, ndiyo iliyotumiwa kwenye kisa ambapo mfanyabiashara Naushad Meralli alilaghaiwa Sh10 milioni na watu walioiga sauti ya Rais.

Hasira zilipanda na majimbizano makali yakazuka kwa dakika 10 kuhusu madai hayo.

Bw Ombeta alidai mbele ya Hakimu Mwandamizi Peter Ooko kuwa Rais aliwahi kumpigia yeye simu kwa nambari hiyo na wakakazugumza.

“Ni ukweli nambari hii iliyoko kwenye nakala za mashtaka ikidaiwa ilitumiwa na washukiwa hawa ni ya Rais Kenyatta. Niko nayo na ndiyo hii. Nilihifadhi kwenye simu yangu aliponipigia simu nayo,” alisema Bw Ombeta.

Ni wakati huo ambapo Bw Okello aliwaka na kumkabili Bw Ombeta.

“Ikiwa wakili Ombeta anataka kutoa ushahidi kuhusu nambari hii, basi aingie kizimbani nimhoji,” alisema Bw Okello.

Cheche za maneno zilitawala kati yao wawili na ikabidi hakimu aingilie kati kuwazima

“Hata kama unasikia Bw Ombeta anasema maneno yasiyo na maana, inakupasa umpe fursa awasilishe hoja za wateja wake,” Hakimu Ooko alisema.

Hatimaye Bw Okello aliomba msamaha kwa kujimbizana na wakili Ombeta hadharani.

Baada ya mawakili hao kutulia, hakimu aliamuru washukiwa Joseph Waswa, Duncan Muchai, Isaack Wanyakeche Wanyonyi, William Simiyu, David Lukaya Kikuyu, Gilbert Kirunja na Antony Wafula Simiyu wafunguliwe mashtaka ya ulaghai.

Washukiwa hao walifunguliwa shtaka la kufanya njama za kulaghai Sh10milioni kutoka kwa Bw Merali, wakidai walikuwa na uwezo wa kumuuzia shamba katika eneo la Milimani, Nairobi.

Walikanusha mashtaka na kuzuiliwa hadi leo ombi lao la kuachiliwa kwa dhamana litakapowasilishwa na mawakili Ombeta, Nevile Amolo na June Ashioya.

Hakimu alikataa ombi la upande wa mashtaka la kutaka washtakiwa wazuiliwe kwa muda wa siku 10 zaidi, akisema polisi wamekuwa na muda wa kutosha kufanya uchunguzi wao tangu walipowakamata mnamo Ijumaa.

  • Tags

You can share this post!

UFISADI: Nini muhimu kati ya urafiki na taifa?

Wazo la mawaziri wawe wabunge lashika kasi

adminleo