Sina fedha za kuboresha shule, asema mbunge wa Ganze
Na SAMUEL BAYA
MBUNGE wa Ganze katika kaunti ya Kilifi, Bw Teddy Mwambire amesema hana namna kuboresha hali ya shule mbovu zilizo katika eneo hilo kwani hajapokea fedha za maendeleo kutoka kwa serikali kuu.
Huku akikiri kwamba shule nyingi katika eneo hilo ziko katika hali mbaya, alidai zilikuwa katika hali hiyo alipoingia mamlakani mwaka wa 2017 na itabidi zikae hivyo hadi eneobunge litakapopokea mgao wa fedha za Hazina ya Kitaifa ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF) katika kipindi cha kifedha cha mwaka huu.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo kwa njia ya simu, mbunge huyo alisema Shule ya Msingi ya Mangororo ambayo picha zake zimekuwa zikisambazwa mitandaoni zikionyesha watoto wakiwa ndani ya darasa lililofurika maji baada ya mvua, ni mfano tu wa hali halisi.
“Nikisema kuwa katika eneo langu la Ganze kuna shule mbaya watu hudhani ninatania. Nimeshukuru sasa kuona Shule ya Msingi ya Mangororo imewekwa mitandaoni ili kubainishwa ukweli ulioko ndani ya Ganze,” akasema.
“Niko na shule zaidi ya 30 eneo bunge la Ganze ambazo ziko hali mbaya hata zaidi ya Shule ya Msingi ya Mangororo. Tunakubali kejeli ingawa tunachukulia hili kama changamoto kubwa ambayo lazima tukabilliane nayo jino kwa ukucha,” akasema Bw Mwambire.
Aidha Bw Mwambire alisema kufikia sasa bado hajaweza kupata mgao wa kifedha wa NG-CDF mwaka wa 2018/2019.
“Kufikia sasa, sijaweza kupata mgao wa 2018/2019 wa miradi kwa sababu ya makosa yaliyofanywa na mtangulizi wangu. Tumejaribu kutafuta suluhu, hata jana asubuhi nilikuwa kwa afisi za halmashauri ya NG-CDF kufuatilia na nikaona tumepiga hatua kubwa,” akasema Bw Mwambire.
Alidai kuwa alirithi shule hizo zikiwa katika hali mbaya na kwamba sasa atalazimika kuzifadhili katika mgao wa kifedha wa mwaka wa 2019/2020.
“Shule hizo ambazo ziko katika hali mbaya zitakaa hivyo kwa muda hadi pale tutakapopata mgao wetu wa fedha za NG-CDF wa 2019/2020. Tukipata fedha hizo, tumepanga kumalizia miradi yote iliyokwama ama ambayo haikumalizwa baada ya kuanzishwa na mtangulizi wangu,” akasema.
Alisema kuwa kwa miradi hiyo yote kukamilika inahitaji takriban Sh65 millioni.
Alitaja shule nyingine ambazo ziko katika hali mbaya kuwa kuwa kama Ranch, Kenga Dalo, Muryachakwe, Mbwana, Kikwanguloni, Tandia miongoni mwa shule zengine nyingi.
“Ni lazima sisi kama wakazi wa Ganze tujumuike kwa harakati za kutafuta mbinu badala ya kupata raslimali za kukwamua hali hii. Tutafute suluhu badala ya kejeli kwani hata mshahara na marupurupu ninayopata haiwezi kushughulikia mambo kama yalivyo nyanjani. Ganze hawezi jengwa na mbunge pekee ila ni kwa wakazi wote,” akasema.
Alisema kuwa licha ya kukosa madwati na majengo duni, taasisi zengine hazina kabisa vifaa na kwambqa watoto wanalazimika kusomea chini ya miti.
“Hivi kunaponyesha, kuna wanafunzi wengie wamebakia majumbani kwa kukosa madarasa, hii bila shaka ni hali ya kusikitisha mno,” akasema mbunge huyo.