Habari Mseto

Soko la vyakula hasa mazao labomolewa Githurai

August 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

WAFANYABIASHARA wa soko la bidhaa za kula Githurai wanakadiria hasara ya kubwa baada ya maduka na vibanda vyao kubomolewa usiku wa kuamkia jana, Jumatano.

Soko hilo ni maarufu katika uuzaji wa matunda, viungo vya mapishi na bidhaa zingine mbichi za kula.

Limepakana na reli, na wengi wa walioathirika ni walio kandokando mwa barabara hiyo ya garimoshi.

Kwa mujibu wa maelezo ya wafanyabiashara tuliozungumza nao, walipewa notisi ya siku tatu pekee kuondoka.

“Tulipewa ilani ya kuondoka siku tatu zilizopita, jambo ambalo limetupa ugumu kujipanga kutafuta njia au sehemu mbadala kuzimbua riziki. Ubomozi ulifanyika usiku wa manane,” akasema Julia Wangari, ambaye anafanya uuzaji wa maparachichi na ndizi.

Mfanyabiashara huyo aliambia Taifa Leo kwamba anakadiria hasara ya mali yasiyopungua thamani ya Sh50, 000. “Isitoshe, ninadaiwa kodi ya nyumba ya miezi mitatu. Nitalisha watoto wangu vipi?” akahoji mama huyo wa watoto watatu.

Baadhi walisema wana mikopo kwenye benki, wakishangaa watakavyomudu kuilipa. “Benki inanidai mkopo wa Sh150, 000 niliochukua kupiga jeki biashara yangu. Maisha yamekuwa magumu wakati huu wa corona, tunakochumia riziki tumefukuzwa na kuharibiwa bidhaa na mali,” akalalamika Veronica Nzioki, mama wa watoto wanne.

Licha ya kujaribu kushirikisha viongozi waliochaguliwa eneobunge la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, kuzuia ubomoaji wa soko la Githurai, juhudi zao hazikufua dafu. James Kiambi alisema diwani wa eneo hilo aliwaambia hana uwezo kusimamisha shughuli hiyo, naye mbunge wa Ruiru Simon King’ara akiwaelekeza kwa shirika la reli.

“Gavana wa Kiambu James Nyoro hakuzungumza na viongozi wetu tuliowatuma kutuwasilishia malalamishi na maombi yetu,” Bw Kiambi akasema, akieleza kwamba wafanyabiashara walioathirika hawakukataa kuondoka, ila wanaomba kuongezewa muda kutafuta sehemu mbadala kuzimbua riziki.

“Ni jambo la kusikitisha serikali kutuhangaisha wakati janga la Covid-19 linatesa watu,” akasema mfanyabiashara huyo akikadiria kupoteza bmali na bidhaa za maelfu ya pesa.

“Tumepoteza mali ya maelfu na mamilioni ya pesa, tunaomba kufidiwa ili tuweze kuimarika tena,” Mophat Kamau akasema.

Ubomoaji wa soko hilo ulijiri siku moja baada ya soko la Mutindwa kubomolewa. Matingatinga yaliyosimamiwa na maafisa wa polisi yalitumika kufanya ubomoaji huo, na kuharibu bidhaa za kula.

Soko la Githurai linakadiriwa kuwa na zaidi ya wafanyabiashara 1, 000, wengi wakidai wamekuwa katika eneo hilo kwa muda usiopungua miaka 10.

Shirika la reli linaendelea kufanya ukarabati wa reli inayounganisha Nairobi na Nanyuki, ili kufufua usafiri na uchukuzi wa mizigo kwa njia ya garimoshi.