• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Somalia yatishia kufurusha KDF nchini humo

Somalia yatishia kufurusha KDF nchini humo

Na AGGREY MUTAMBO

UHUSIANO wa Kenya na Somalia umeendelea kuzorota huku Rais Mohamed Abdullahi Farmaajo akitisha kuwatimua wanajeshi wa Kenya (KDF) wanaohudumu nchini humo chini ya kikosi cha Muungano wa Afrika (Amisom).

Viongozi wa mataifa ya eneo hili chini ya mwavuli wa IGAD, walifanya mkutano wao wa 38 nchini Djibouti, Jumapili na suala la kudorora kwa uhusiano wa Kenya na Somalia lilitarajiwa kujadiliwa.

Tishio la kuwatimua maafisa wa KDF linafuatia kufukuzwa kwa Balozi wa Kenya nchini Somalia.

Mnamo Ijumaa, Waziri wa Ulinzi Bi Monica Juma alifutilia mbali kikao na wanahabari katika makao makuu ya kijeshi (DoD) dakika za mwisho.

“Maandalizi yote yalikuwa yamefanywa lakini Bi Juma hakufika,” afisa mkuu wa KDF alieleza Taifa Leo.

Farmaajo anataka wanajeshi wa Eritrea wachukue pahala pa wanajeshi wa KDF katika Amisom.

“Kuweko kwa maafisa wa KDF nchini Somalia kunadhibitiwa na mikataba ya Amisom,” Kanali Zipporah Kioko, ambaye ni msemaji wa KDF alisema.

Kwa mujibu wa mikataba hiyo, nchi ambayo inapokea misaada ya kijeshi kutoka mataifa mbali mbali haiwezi kuwatimua wanajeshi wa kulinda amani.

Somalia imeshirikisha maafisa kutoka mataifa wanachama wa Amisom kuiunga mkono katika jitihada zake za kusitisha uhusiano na Kenya.

Wakati wa mkutano huo Djibouti suala hili la uhusiano baina ya Kenya na Somali lilinuiwa kupatiwa kipaumbele.

Somalia inalaumu Kenya kwa kuingilia masuala ya ndani, hasa uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwakani.

  • Tags

You can share this post!

Watford wampa Xisco Munoz mikoba yao ya ukocha

OMAUYA: Diplomasia: Rais wa Somalia asichagulie Kenya...