Somo la usalama barabarani kuanza kufundishwa
Na CHARLES WASONGA
WANAFUNZI wa shule za msingi na upili watafundishwa kuhusu usalama barabarani kama somo mahsusi kwenye mtaala kuanzia mwaka ujao ikiwa serikali itatekeleza hoja iliyowasilishwa Jumatano bungeni.
Hoja hiyo iliyowasilishwa na Mbunge wa Mugirango Kusini, Silvanus Osoro, pia inapendekeza kuwa somo hilo litahiniwe pamoja na masomo mengine kama njia ya kuhakikisha wanafunzi wanalichukulia kwa uzito.
Kwa kauli moja, wabunge waliunga mkono hoja hiyo wakisema somo hilo litaimarisha ufahamu kuhusu sheria za barabarani miongoni mwa wanafunzi, na kupunguza ajali za barabarani.
“Japo kuna sheria nyingi za usalama barabarani nchini, utekelezaji wa sheria hizo ungali changamoto kubwa. Hii ndiyo sababu wananchi wengi wameendelea kuuawa, kujeruhiwa na kulemazwa katika barabara zetu,” akasema Bw Osoro.
“Ndiposa ni muhimu kwa wanafunzi kufunzwa kuhusu usalama wa barabara shuleni kama njia ya kupunguza ajali zinazotokana na ukosefu wa ufahamu kuhusu sheria za hizo,” akaongeza.
Takwimu zinaonyesha kuwa kwa wastani watu 3,000 hufariki kutokana na ajali za barabarani kila mwaka nchini huku wengine wengi wakijeruhiwa.
Kulingana na Bw Osoro, japo Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Barabara (NTSA) imepewa wajibu wa kuunda mikakati ya kuhamasisha umma kuhusu usalama barabarani, haijatekeleza wajibu huo kwa njia inayoridhsha.
Akiunga mkono hoja hiyo, Mbunge Maalum David Sankok aliitaka serikali kutekeleza mapendekezo ya hoja hiyo, akisema yatapunguza pakubwa ajali ambazo huangamiza wengi katika barabara nchini.
Wengine waliochangia hoja hiyo ni wabunge John Mbadi (Suba Kusini), Dkt Robert Pukose (Endebess), Gladwel Cheruiyot (Baringo), Nixon Korir (Langata), Christine Ombaka (Siaya) kati ya wengine.
Bw Mbadi aliitaka Wizara ya Elimu kuhakikisha kuwa somo la usalama barabarani linajumuishwa katika mtaala mpya.