Habari Mseto

Sonko na Passaris waelekea kuridhiana tena

July 20th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KUNA dalili kwamba Gavana wa Nairobi, Mike Sonko na Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti hiyo, Esther Passaris kupatana tena baada ya kukosana Juni 2019.

Hii ni baada ya wawili hao kuandamana Jumamosi na Rais Uhuru Kenyatta katika hafla ya uzinduzi wa Kiwanda cha Kampuni ya Maziwa ya KCC, Mowlem, Dandora, Nairobi.

Katika mojawapo ya picha zilizopigwa katika hafla hiyo, viongozi hao wawili wa Nairobi wanaonekana wakishiriki mazungumzo, ishara kwamba wameridhiana.

Mnamo Juni 1, 2019, Sonko na Passaris walizomeana hadharani katika uwanja wa Shule ya Upili ya Pumwani ambako sherehe za Jamhuri ziliandaliwa.

Gavana Sonko alimkaripia vikali Bi Passaris, pale mwakilishi huyo wa wanawake alilalamika hadharani kwamba gavana huyo hukosa kujibu simu zake wala kushauriana naye katika masuala yanayowahusu wakazi wa Nairobi.

Hatua hiyo ilisababisha Bi Passaris kuondoka kutoka hafla hiyo kwa hasira huku akilalamika kuwa Bw Sonko alimkosea heshima kwa kumdhalilisha mbele ya umma.

Mahojiano yazimwa

Bw Sonko aliendelea kumshutumu Bi Passaris katika runinga ya Citizen TV kwa kutumia maneno ya ‘aibu’.

Ni hali iliyowalazimisha wasimamizi wa kipindi hicho kuzima mahojiano hayo.

Vita vya maneno kati ya Sonko vilikera zaidi kiasi cha kulazimisha serikali kupitia Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia kutoa taarifa ikilaani kile ilitaja kama mtindo mbaya wa kushambulia na kuwadunisha viongozi wanawake.

Na bungeni, wabunge wa kike wakiongozwa na Mbunge wa Suba Kaskazini Bi Millie Odhiambo walimtetea Bw Sonko kwa kumkosea heshima Bi Passaris.

Sasa inaonekana kuwa uhasama na joto la uadui kati yao limepungua na wanaweza hata kuzungumza katika halfa ya hadhara.