Habari Mseto

Spika wa bunge la Kitui na madiwani 4 wafurushwa hotelini na wahuni waliokodishwa

Na MWANDISHI WETU December 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

HASIRA zilipanda katika hoteli moja mjini Kitui Jumatano usiku wakati wahuni wanaoaminika kukodishwa na wanasiasa walipomvamia na kumfedhehesha spika wa bunge la Kitui Kevin Kinengo na madiwani wanne kabla ya kuwatimua kutoka hoteli hiyo.

Wanaume kadhaa waliingia kwenye chumba cha watu mashuhuri cha hoteli hiyo na kiongozi wa kikundi hicho akaamrisha Kinengo na  madiwani hao kuacha mara moja walichokuwa wakifanya na kuondoka bila kuuliza swali au kupinga.

Katika video iliyosambazwa, sauti ya mwanamume inasikika ikimwambia spika na madiwani kwamba hawangewadhuru ikiwa wangetii maagizo na kuondoka kwa haraka na kwa amani.

“Ondoka, ondoka sasa,” mwanamume huyo alimfokea Kinengo na kundi lake. Spika, naibu wake na MCA wa Kyangwithya Magharibi, Christopher Nzilu, kiongozi wa wengi wa bunge na MCA wa Migwani Harrison Maluki, MCA wa Mwingi ya Kati Bernard Sila na MCA wa kuteuliwa wa Wiper Priscilla Makumi walinyanyuka kwenye viti vyao na kuondoka.

Kinengo alitoa taarifa kwa vyombo vya habari ambapo alithibitisha kweli walivamiwa na wahuni katika hoteli hiyo ya kifahari inayomilikiwa na gavana wa chama cha UDA wa kaunti moja.

“Ninathibitisha kuwa Jumatano, Desemba 11 2024, mwendo wa saa nne usiku, tulipokuwa tukila chakula cha jioni na baadhi ya waheshimiwa madiwani katika hoteli moja katika mji wa Kitui, tulivamiwa na wahuni ambao walitufurusha kutoka hotelini kwa njia ya kusikitisha,” Spika alisema.

Hata hivyo, alithibitisha yeye na wenzake wako salama, na watachukua hatua zinazohitajika kisheria.

“Ninalaani vikali unyanyasaji wa raia yeyote wa Kenya, haswa viongozi, wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria. Ninaomba amani na utangamano katika kaunti yetu kuu ya Kitui. Mungu ibariki Kaunti ya Kitui,” Kinengo alisema kwenye taarifa hiyo.

Shambulio hilo limetokea wakati kumekuwa na vita vya maneno kati ya spika na Gavana Julius Malombe.

Wiki iliyopita, Kinengo na Dkt Malombe kila mmoja alidai kuwa mwenzake ndiye aliyechangia kwa uhusiano baridi kati ya bunge na serikali ya kaunti.

Siku ya Jumatano, kamati ya uchunguzi ya bunge ya kaunti iliyochunguza ukiukaji wa katiba na utovu wa nidhamu dhidi ya waziri wa kaunti anayehusika na fedha Peter Kilonzo almaarufu Tangawizi ilimpata na hatia ya mashtaka na kuamuru afike mbele ya kikao cha Jumanne ili kujitetea.

Katika hoja hiyo iliyotayarishwa na Mwakilishi wa Wadi ya Kiomo/Kyethani, Antony Musyoka, Bw Kilonzo, miongoni mwa mambo mengine, anadaiwa kukiuka Katiba, uzembe, matumizi mabaya ya afisi na utovu wa nidhamu uliokithiri.