Spika wa Kitui asimulia alivyozuiliwa Dubai sababu ya deni la serikali ya Ngilu
SPIKA wa Bunge la Kaunti ya Kitui Kelvin Kinengo, alizuiliwa na serikali ya Dubai kwa wiki mbili kwa madai ya kutolipa deni la kaunti la Sh8.9 milioni.
Bw Kinengo ambaye alikuwa Dubai kwa shughuli rasmi za Bunge alizuiwa kusafiri kurejea Kenya jioni ya Jumatano Julai 10 baada ya polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai kutekeleza agizo la mahakama la kuzuia maafisa wakuu wa Kaunti ya Kitui kusafiri.
Spika alilazimika kukaa Dubai kwa siku kumi na tano hadi Alhamisi Julai 25, aliporuhusiwa kusafiri baada ya maafisa wa Kaunti waliorejea nyumbani kulipa deni hilo na agizo likaondolewa.
Alizuiwa kusafiri nyumbani baada ya kampuni ya Ushauri ya Dubai iliyohusika kuandaa maonyesho ya Dubai Expo 2021, kwenda Mahakamani mwaka 2021 na kufanikiwa kupata amri ya kuzuia maafisa wakuu wa kaunti ambao wangepitia Dubai hadi deni lilipwe kikamilifu.
Kampuni ya TBLDC Group ilidai katika stakabadhi zilizoonwa na Taifa Leo kwamba Kaunti ya Kitui iliwapa kandarasi ya kuwezesha aliyekuwa Gavana Charity Ngilu na ujumbe wa maafisa 15 kushiriki katika Maonyesho ya Dubai ya 2021, yaliyoanza Oktoba 17 hadi 26, mwaka huo.
Wakili wa Kaunti hiyo Timothy Mwange alikataa kuzungumzia suala hilo lakini mahojiano na maafisa kadhaa ambao hawakutaka kutajwa majina kutokana na joto kali la kisiasa lililotokana na suala hilo, walithibitisha kwamba suala hilo halikushughulikiwa hata kidogo licha ya idara ya sheria kuitwa kuhudhuria vikao vya mahakama Dubai.
“Ofisi ya Mwanasheria wa Kaunti ilipokea stakabadhi za kesi hiyo zilizoandikwa kwa Kiarabu lakini haikufasiriwa kwa Kiingereza kuelewa msingi wa kesi mahakamani,” alisema afisa mkuu anayefahamu kuhusu suala hilo.
Kampuni hiyo ilidai mahakamani kwamba ililipa ada ya usajili ili maafisa wa kaunti ya Kitui washiriki katika Maonyesho ya Dubai, bili za hoteli, tiketi za ndege na huduma zingine kwa gharama ya Sh8.9 milioni.
Ujumbe wa watu 16 wa Gavana Ngilu kwenye maonyesho ya siku tisa ya Dubai ulijumuisha Spika wa Bunge wakati huo George Ndotto, mawaziri wawili wa Kaunti, Maafisa Wakuu wawili na madiwani tisa wa Bunge la Kaunti.
Katika mahojiano na Taifa Leo, Spika huyo kijana alisimulia masaibu ya kuzuiliwa katika nchi ya kigeni kutokana na makosa ambayo hajui lolote kuyahusu.
Awali, alizungumza hadharani kuhusu suala hilo wakati wa maonyesho ya kila mwaka ya Kilimo na Biashara ya Kitui katika uwanja wa maonyesho wa Ithookwe.
“Sikuwa chini ya ulinzi wa polisi wa Dubai, nilikuwa huru kwenda popote ndani ya jiji lakini sikuweza kuondoka nchini kwa kuwa maelezo yangu yalikuwa yamesambazwa katika sehemu zote za kuondoka nchi hiyo,” alisema Bw Kinengo na kuongeza marufuku ya kusafiri iliondolewa tu baada ya kampuni kupokea haki yake.
Spika Kinengo, ambaye ni mwanasheria kitaaluma alisema haikuwa rahisi kujua ni kwa nini alizuiwa kwa sababu katika Milki za Kiarabu, kuna siku nne tu za kazi ambazo zinaanzia Jumapili hadi Alhamisi.
“Niliwasiliana na Gavana Julius Malombe na kumweleza kuhusu hali yangu, naye aliitisha kikao cha dharura cha baraza la mawaziri ili kusuluhisha suala hilo,” alifafanua na kuongeza kuwa aliruhusiwa tu kupanda ndege iliyopangwa upya hadi Nairobi baada ya kaunti kulipa deni na Mahakama ikaondoa amri ya kumzuia kusafiri.