Habari Mseto

SUPKEM yakana kudinda kulipa maajenti waliofanikisha Hija

October 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na CECIL ODONGO

BARAZA la Dini ya Kiislamu nchini, SUPKEM limejitokeza Jumatatu na kukanusha vikali madai kwamba limewakatalia fedha za maajenti waliosimamia na kufanikisha safari za mahujaji kwa ibada za Hija 2018.

Akijibu madai yaliyotolewa na wengi wa maajenti wanaoendelea kuwaandama kuhusu malimbikizi ya madeni, uongozi wa baraza hilo umesema ni ajaenti moja tu aliye na haki ya kulipwa fedha zisizozidi Sh4 milioni na kuwataka wengine wanaohisi wameonewa kufika katika ofisi zao ili waonyeshwe jinsi mapeni yao yalivyowajibishwa.

Naibu Mwekahazina wa SUPKEM Abdallah Ali katika mahojiano na Taifa Leo alidai maajenti wengi hawaelewi kwa kina mchakato mzima na sheria mpya zilizoasisiwa na serikali ya Saudi Arabia zilizoanza kutumika mwaka huu.

“Nawaomba wato wanaosema wanatudai wafike kwetu na wawasilishe stakabadhi zao nasi tuwafafanulie kila suala kwa mapana na marefu kulingana na sheria mpya zilizoongoza hajj ya mwaka huu. Ni kampuni ya Zaky travelling agencies ndiyo tunafahamu wana kesi yenye mashiko ila pesa zao hazifiki 16milioni jinsi wanavyodai,” akasema Bw Ali.

Vile vile aliwakashifu na kulaumu maajenti wanaowalaghai Waislamu kutoka mataifa jirani ili kufanikisha zafari zao za hajj bila kuhakikisha wanapata stakabadhi muhimu kama vibali vya kazi kutoka kwa serikali, pasipoti na chanjo za maradhi.

“Lazima nifunguke na niseme kwamba baadhi ya wanoapiga kelele walichukua pesa za raia kutoka Somalia na Ethiopia na wakatimiza masharti mengine za kisheria lakini kimaksudi wakakosa kupata vibali vya kazi kutoka serikali kwa wateja wao. Sasa wanapodaiwa wanatusingiza ilhali lengo lao kuu ni kuponyoka na fedha hizo wala sisi hatukuchangia safari hizo kutibuka,” akaongeza Bw Ali.

Aidha alipuuza ripoti zilizoibuka za huduma duni kwa waliokwenda hajj kusema kwamba kulikuwa na kisa kimoja tu cha muumini aliyelemewa na bado anaendelea kupata matibabu nchini Saudia hadi hali yake iimarike ndipo arejee.

“Huyo mwenzetu hajarejea nchini kwasababu anaendelea kutibiwa na tunafuata maendeleo yake kwa ushirikiano na serikali ya huko. Mahema, usafari na mahitaji ya kimsingi ya kila mtu yalishughulikiwa vizuri sana,’ akasisitiza Bw Ali.

Hata hivyo kilichojitokeza ni ubabe wa uongozi kati ya viongozi wa sasa wa baraza hilo na waliokuwa viongozi wa awali, hali ambayo kulingana na Bw Ali isipodhibitiwa itazidi kuibua mgawanyiko mkubwa kati ya Waislamu.