Tabasamu kwa wanafunzi Helb ikitoa Sh13.7b kufadhili masomo
Na Faith Nyamai
HATIMAYE Bodi ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu (HELB) imetoa Sh 13.7b kufanikisha elimu ya wanafunzi 296,604 katika mwaka wa kifedha wa 2018-2019.
Kulingana na Afisa Mkuu wa HELB Charles Ringera, wanafunzi wanaotegemea mikopo hiyo wameongezeka kwa asilimia 97 katika muda wa miaka mitano iliyopita huku kiwango cha ukuaji wa kuisambaza mikopo hiyo kikipanda kwa asilimia 70 katika kipindi hicho.
“Tangu kuanzishwa kwake, Helb imetoa Sh 84bilioni kama mikopo kwa wanafunzi 671,448 huku wengine 396,329 wakiwa wamefikia muda wa kuilipa mikopo waliyopewa inayokadiriwa kuwa Sh 47bilioni,” akasema Ringera.
Habari nzuri hata hivyo ni kuwa Wakenya 190,554 waliopewa mikopo hiyo miaka ya nyuma wamekamilisha malipo yao ya Sh18.2b ilhali wengine 144,075 wanaendelea kulipa kiasi cha Sh22.1b wanachodaiwa.
Wakati huo bodi ya Helb imetoa wito kwa vyuo husika kuanza kutumia mbinu ya kadi ya malipo maarufu kama smart cards ili kuwawezesha kudhibiti mikopo ya Helb kwa wanafunzi wao.