• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 2:53 PM
Tabichi ateuliwa balozi wa kuwatetea watoto duniani

Tabichi ateuliwa balozi wa kuwatetea watoto duniani

Na SAMWEL OWINO

MWALIMU bora duniani, Peter Tabichi ameteuliwa balozi wa kuendelesha kampeni ya elimu ya watoto katika mataifa yanayokumbwa na vita na mizozo na asasi ya kimataifa, mwezi mmoja baada ya kutawazwa na Varky Foundation.

Katika wajibu huu mpya, Bw Tabichi ambaye ni mwalimu wa Hisabati na Fizikia katika Shule ya Upili ya Keriko, iliyoko kaunti ya Nakuru, atatetea masilahi ya zaidi ya watoto 75 milioni kote ulimwenguni ambao masomo yao huvurugwa na mapigano na majanga ya kimaumbile.

Kwenye taarifa, wakfu huo ulitesema utategemea sifa alizopata Bw Tibichi ulimwenguni, kuelezea haja ya kuwekeza katika mipango ya kulinda mustakabali wa watoto wanaokabiliwa na changamoto hizi.

Mkenya huyo sasa ataungana na waigizaji wengine maarufu kama vile Will Smith na Rachel Brosnahan ambao ni watetezi wa masilahi ya watoto chini ya shirika la “Education Cannot Wait” ambalo huendesha kampeni ya kuhakikisha kuwa watoto katika mataifa yanayokumbwa na mizozo wanapata elimu.

Kwa hivyo, sawa na wasanii hao wawil, Bw Tabichi pia atakuwa akizunguka katika mataifa ambako watoto wanateswa kufuatia mizozo ili kuendesha kampeni za kuhimiza wapesa nafasi ya kusoma.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown, ambaye ni Balozi Maalum wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu Elimu Ulimwenguni na mwenyekiti wa kamati Simamizi ya Shirika la Education Cannot Wait, alimtaja Bw Tabichi kama kielelezo chema kwa wale wote wanaohusika katika shughuli za kutoa mafunzo.

Bw Brown alisema yuko tayari kufanya kazi na Mkenya huyo ili kuendesha ajenda muhimu ya kuhakikisha kuwa watoto katika mataifa yenye changamoto wanapata elimu.

Katika hotuba yake ya kukubali uteuzi huo, ambao kwa mara nyingine umemweka katika ramani ya ulimwengu, Bw Tabichi alitaja uteuzi huo kama heshima kuu.

“Uteuzi huu unaashiria namna ambayo ulimwengu unatathmini kazi yangu kama mwalimu. Ni heshima kuu na ninaahidi kuwasaidia watoto ambao maisha yao yanaathiriwa na vita pamoja na majanga mengine,” akasema.

“Inavunja moyo kujua masomo ya zaidi ya watoto 75 milioni kote ulimwenguni huvurugwa na vita pamoja na majanga ya kimaumbile. Itakuwa ni wajibu wangu kuhakikisha kuwa maisha ya watoto hao yanaimarika kwa kupata elimu bora,” Bw Tabichi akaeleza,

You can share this post!

Pasta ndani kuhubiri Huduma Namba ni ya kishetani

Nyumba 50 zateketea Mukuru-Kaiyaba

adminleo