‘Tafuteni basari za watoto kule mlipiga kura’
NA TITUS OMINDE
MAMIA ya wanafunzi wasio na hatia na kutoka familia maskini katika eneobunge la Soy, Kaunti ya Uasin Gishu huenda wakakosa kuendelea na elimu yao kwa kukosa basari.
Mbunge wa Soy David Kiplagat ametenga kitita cha Sh7 milioni za masomo lakini kundi hilo la wanafunzi halitanufaika kutokana na pesa hizo kwa sababu ya ‘dhambi’ iliyofanywa na wazazi wao wanaodaiwa kupiga kura katika eneobunge jirani la Likuyani, Kaunti ya Kakamega.
Bw Kiplagat ameapa kutozingatia wanafunzi ambao wazazi wao walijiandikisha kuwa wapigakura katika eneobunge la Likuyani wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.
Bw Kiplagat aliwaambia wazazi na walezi wa wanafunzi walioathiriwa kutafuta usaidizi wa kifedha kwa watoto hao Likuyani ambako alidai kuwa walipiga kura kuchagua viongozi katika eneobunge hilo.
“Mwanafunzi yeyote ambaye mzazi na mlezi wake alipiga kura katika eneobunge la Likuyani, hatanufaika na mgao wetu wa hazina ya busari,” akasema Bw Kiplagat.
Akiongea katika afisi ya Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF) ya eneobunge la Soy mjini Eldoret mnamo Jumatano, Januari 3, 2024, wakati wa utoaji wa hundi ya Sh7 milioni kusaidia wanafunzi kutoka familia zinazohitaji kupigwa jeki katika wadi tano, mbunge huyo alisema kupitia kwa mtaalamu wake wa tekinolojia ya mawasiliano, aligundua vyema kuwa wazazi wa wanafunzi walioathiriwa walipiga kura kuchagua viongozi huko Likuyani.
Bw Kiplagat ambaye ni mbunge wa muhula wa kwanza, alisema kuwa wazazi ambao hawatajiandikisha kuwa wapigakura katika eneobunge lake watawanyima watoto wao haki ya kunufaika na basari hiyo chini ya NG-CDF.
“Baadhi ya wazazi wanalia kwa uamuzi ambao si wetu bali ni wao. Yangu ni kusikitikia tu masaibu ya watoto wao lakini ikiwa wanataka basari kwa watoto wao, wanapaswa kwenda kuipata mahali wanapopiga kura kila wakati wa uchaguzi,” aliongeza.
Bw Kiplagat alisema kuwa kwa ujuzi wake katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, alienda katika afisi ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) eneobunge la Soy kukagua ikiwa wengi wa wazazi waliotuma maombi ya ufadhili wa watoto wao ni wapigakura wanaofaa katika eneo lake.
Hata hivyo, kwa mshtuko, aligundua kuwa wengi wao walikuwa wakazi wa Soy lakini waliojiandikisha kama wapigakura katika eneobunge la Likuyani.
Alisema kuwa rekodi za IEBC zimemwezesha kutambua wapigakura ‘matapeli’ ambao watoto wao hawapaswi kunufaika na hazina hiyo.