Habari Mseto

Tahadhari mgonjwa akipatikana na homa ya nyani

Na WINNIE ATIENO August 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WIZARA ya Afya imeanza kusaka Wakenya waliotangamana na dereva mmoja wa masafa marefu ambaye anaugua homa ya nyani.

Kenya ilithibitisha kisa cha kwanza cha virusi vya homa ya nyani inayofahamika kama mpox katika mpaka wa Taita Taveta na Tanzania.

Kulingana Katibu wa Wizara ya Afya Bi Mary Muthoni, dereva huyo alisafiri kutoka Kampala nchini Uganda hadi Mombasa, na baadaye kwenda Rwanda kupitia mpaka wa Taita Taveta na Tanzania.

Dereva huyo anaendelea na matibabu humu nchini.

Kuzuia kusambaa kwa homa hiyo haraka, serikali imeanza kusaka wale wote ambao huenda walitangamana na dereva huyo ili waanze kupokea matibabu.

Bi Muthoni alisema wizara yake inasaka waliotangamana na mgonjwa huyo, anakofanya kazi, hospitali alikolazwa na kule alikosafiri.

Hata hivyo, Bi Muthoni aliondoa wasiwasi kuhusu ugonjwa huo akisema Kenya imenakili kisa kimoja tu.

“Tunaendelea kumchunguza dereva huyo. Kufuatia kutua kwa ugonjwa huo hapa nchini, wizara ya afya imechukua hatua madhubuti kuzuia usambazaji ikiwemo kusaka waliotangamana na dereva huyo,” akasema Bi Muthoni.

Katibu huyo, alisema uchunguzi wa kimatibabu umeimarishwa hasa katika mipaka ya Kenya, barabara kuu ya Busia kuelekea Mombasa na Taita Taveta.

Vile vile, serikali inashirikiana na nchi jirani ambako dereva huyo alisafiri kusaka wale ambao walitangamana naye.

Alisema serikali za kaunti pia zimehamasishwa kuhusu homa hiyo na namna ya kukabiliana nayo.

Katika kaunti za Mombasa na Taita Taveta, wahudumu wa afya wamewekwa kwenye hali ya tahadhari kufuatia homa hiyo.

Katika hospitali kubwa zaidi eneo la Pwani, wakuu wa afya wameimarisha kitengo cha dharura ambako yeyote atakayepatikana na homa hiyo atalazwa na kutibiwa.

Kulingana na wataalamu wa afya, maambukizi hayo ambayo husababishwa na virusi vya mpox ambavyo huenea watu wanapotangamana kwa karibu na husababisha dalili za mafua na upele.

“Tunasihi Wakenya wanawe mikono mara kwa mara ili kupunguza hatari ya kuambukizwa. Ukiwa na dalili yoyote inayohusiana na virusi hivyo, tafadhali njoo hospitalini kwa matibabu, epuka kutangamana kwa karibu na watu wengine,” alisema afisa wa afya ya umma Rukiya Abdulrahman.

Baadhi ya dalili zake ni pamoja na upele, kuumwa na kichwa, kuumwa na mgongo.

Dalili hizo husalia mwilini kwa wiki mbili hadi nne. Abdulrahman aliwasihi wakazi kutotangamana na wale ambao wana dalili za ugonjwa huo na badala yake akawataka wakazi kuvaa barakoa kila mara.