Habari Mseto

Taifa ambako wanawake hutungoza wanaume Valentino Dei

February 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

MAENEO tofauti kote duniani huadhimisha siku ya Valentino kwa njia tofauti, nyingine za kimapenzi na zinazoonekana kuwa za kawaida na nyingine za kipekee.

Japo ni utamaduni ambao haujakita mizizi ipasavyo nchini Kenya na ambao sasa unaanza kuenziwa na kizazi cha vijana wa sasa, ni wazi kuwa mataifa mengi haswa ya magharibi mwa dunia yamekuwa yakisherehekea sikukuu hii kwa karne nyingi.

Nchini Denmark, siku hii huadhimishwa kwa wanaume kuwatumia wanawake wanaowapenda vijikaratasi vilivyoandikwa shairi ama kichekesho.

 

Ikiwa mwanamke mlengwa atajua aliyemtumia kijikaratasi hicho, anajishindia yai lililopikwa kwa njia spesheli, baadaye mwaka unaposonga.

Vilevile, raia wa Denmark hutumia siku hiyo kubadilishana kadi zenye jumbe za mapenzi na wapenzi wao.

Nchini Korea Kusini nako, ni wanawake ambao huwatongoza wanaume kwa kuwazawadi kwa maua, chokoleti na zawadi nyingine siku hii. Wanaume nao mwezi baadaye, kila Machi 14, hufanya hisani kwa ukarimu waliopata na kuwazawadi wanawake hao.

Nchi hii ni ya kipekee ambapo baada ya wapendanao kusherehekea mapenzi yao Februari na Machi 14, wasio na wapenzi nao huwa na siku yao mwezi baadaye, Aprili 14, ambapo huwa wanaomboleza upweke wao kwa kula vyakula viitwavyo dark bowls (jajangmyeon) ama black bean-paste noodles.

Nchini Ufilipino nako siku hii ina umaarufu mkubwa na raia wake huitumia kwa njia spesheli, ambapo harusi za halaiki huandaliwa.

Hapa barani Afrika, nchini Afrika Kusini wanawake hupachika majina ya wanaume wanaowapenda kwenye mikono ya blausi, hata ikiwa wanaume hao hawafahamu. Majina hayo huandikwa katika vitu vilivyochongwa kuwa muundo wa moyo.

Nchini Wales, watu husherehekea Valentino kwa kutuzana zawadi za vijiko vya mbao. Ni utamaduni ulioanza karne nyingi zilizopita na vijiko hivi huthaminiwa sana, kwani hata huwa zawadi wakati wa harusi.

Nchini Ujerumani, wapenzi huwa hawazawadiani kwa chokoleti, maua na zawadi zenye umbo la moyo tu, mbali pia hupeana zawadi za nguruwe. Nguruwe katika sherehe hizi huwa ishara ya bahati na anasa na zinaweza kuwa kwa njia ya mchoro ama mchongo.

Nchini Italia, wapendanao hupatana kujiburudisha kwa nyimbo, ushairi na kuzawadiana. Aidha, wapenzi hupeana nukuu za kimapenzi zikiwa zimechapishwa katika vijikaratasi. Kulingana na utamaduni wa Italia, mwanamume wa kwanza ambaye msichana anakutana naye siku hii ndiye atakuwa mumewe na kabla ya mwaka kuisha watakuwa wameoana.

Nchini Taiwan, ubadilishanaji wa maua ni ishara kubwa ya mapenzi. Hata hivyo, kulingana na idadi na rangi ya maua anayotoa mwanaume kwa mwanamke, maana huwa tofauti kuhusu aina ya uhusiano baina yao.