Tambua sababu za wakazi Nairobi kupimiwa maji licha ya mabwawa kujaa pomoni
NA HILARY KIMUYU
WAKAZI wa Kaunti ya Nairobi wataendelea kutumia fedha nyingi ili kupata maji, baada ya kampuni ya kusambaza maji jijini kusema itaendelea kutoa bidhaa hiyo kwa vipimo.
Kinaya ni kuwa, hilo ni licha ya mabwawa mengi nchini kujaa maji hadi pomoni, kutokana na mvua kubwa ambayo imekuwa ikiendelea kunyesha.
Jumapili, Kampuni ya Kusambaza Maji ya Jiji la Nairobi (NCWSC), ilisema itaendelea kusambaza maji kwa vipimo kwa wakazi, inapoweka mikakati ya kuboresha usafi wa kiwango kidogo cha maji kilichopo.
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Bw Nahashon Muguna, alisema mpango wa kusambaza maji kwa usawa utawawezesha wateja kupata maji angaa mara moja kwa wiki.
Alisema kuwa kwa sasa, hitaji la kiwango cha maji jijini kwa siku ni lita 900 milioni, ingawa mitambo ya maji ya kampuni hiyo ina uwezo wa kusambaza lita 525.6 milioni za maji kwa siku.
Ijapokuwa mabwawa kama Chemichemi za Kikuyu, Ruiru, Sasumua na Thika yamevunja kingo zake, mitambo ya kutibu maji iliyo katika maeneo ya Ngethu, Sasumua, Kabete na Kikuyu, ina kiwango maalum cha maji ambayo huwa inatibu na kusambaza kila siku. Hivyo, hilo linamaanisha haiwezi kupitisha kiwango hicho.
“Hilo linamaanisha kuwa kama jiji, tunaweza kupata tu kiwango cha maji kinachotibiwa na mitambo hiyo. Kwa hivyo, hata wakati mabwawa yetu yanapofurika, kama ilivyo sasa, kiwango cha maji kinachosambazwa hakitaongezeka. Hatuwezi kupitisha kiwango ambacho mitambo hiyo inafaa kutibu na kusambaza,” akasema.
Mitambo hiyo minne ina uwezo wa kusambaza lita 440 milioni za maji, lita 61 milioni, lita 20 milioni na lita milioni nne mtawalia.
“Mafuriko yanayoendelea jijini yamesomba baadhi ya mirereji ya kusambaza maji, hali ambayo imeathiri sana huduma zetu. Hilo pia limefanya baadhi ya sehemu kupata maji kwa kiwango cha chini,” akaongeza.
Baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa ni Fedha 1, Infinity katika Barabara ya Kangundo, Tumaini, Tassia, Avenue Park 1 na 2, Nyayo Embakasi, Eneo la Barabara ya Kware, Kwa Ndege, Lower Plot 10 na maeneo yaliyo karibu.
Mengine ni Ngomongo, Korogocho, Matopeni-Kayole, Brookeside Grove Westlands, barabara za Wangapala na Iregi– Parklands, Cotton Road, Dennis Pritt Road karibu na Jacaranda, Kambi ya Kijeshi ya Kahawa na Chuo Kikuu cha Kenyatta.