• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
‘Tangatanga’ wadai ipo njama kali kuwatisha wasimuunge Ruto

‘Tangatanga’ wadai ipo njama kali kuwatisha wasimuunge Ruto

Na DENNIS LUBANGA na GRACE GITAU

WABUNGE wanachama wa kundi linaloegemea upande wa Naibu Rais William Ruto wametaka kukomeshwa kwa harakati za kuwatisha baada ya kuibuka madai ipo njama za kutaka kumuua, wakisema kukamatwa kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Kidijitali katika asasi ya urais, Dennis Itumbi, ni njama ya kuwatia uoga wasiunge mkono azma yake ya kugombea urais 2022.

Wabunge walisema Ijumaa hawatatishika na kwamba wataendelea kumpigia debe Dkt Ruto licha ya kile walichodai ni njama ya kuwanyamazisha.

Kulingana na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, kukamatwa kwa Bw Itumbi, ni njama ya kuwatisha watu wanaoaminika kuwa wandani wa Naibu Rais William Ruto.

Akiongea na wanahabari baada ya kuongoza sherehe ya kwanza ya kufuzu ya Wakfu wa Double Impact iliyofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Central katika kaunti ya Uasin Gishu, Bw Nyoro alisema viongozi wanaounga mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022 hawatatishwa na hatua ya kukamatwa kwa Bw Itumbi.

“Kama viongozi wandani wa Naibu Rais, hatutatishwa na mtu yeyote au asasi yoyote kwa sababu tumepitia mengi. Wanaweza kufanya yale wanataka kufanya lakini tunashikilia kuwa taifa hili sharti liNongozwe na mmoja wetu, na huyo si mwingine ila ni Naibu Rais Dkt Ruto,” akasema.

Bw Nyoro alimlaumu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI), George Kinoti, kwa masaibu yaliyomkumba Bw Itumbi, akisema hiyo ni thibitisho kwamba afisi hiyo inashawishiwa na mrengo fulani wa kisiasa.

“Tunataka kumwambia Kinoti akome kusambaratisha taasisi za umma nchini. Hafai kuonekana kufanyia kazi mrengo fulani wa kisiasa kwa sababu sasa ni wazi kuwa hakuna haki katika msururu huu wa kukamatwa kwa watu kwa tuhuma mbalimbali,” aliongeza.

Vile vile, Bw Nyoro alidai kuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga anapanga kusambaratisha chama cha Jubilee.

“Tunataka kuambia upinzani na hasa Bw Odinga kwamba tunajua kile ambacho wanapanga. Lakini wajue kwamba hatutakubali chama chetu cha Jubilee kugawanywa kwa sababu tunalenga mwaka wa 2022 wakati ambapo Rais Uhuru Kenyatta atapokeza Dkt Ruto mamlaka,” akasema.

Hadaa

Naye Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti ya Laikipia katika Bunge la Kitaifa, Bi Catherine Waruguru, alitaja hatua ya kukamatwa kwa Bw Itumbi kama njama ya DCI kuwahadaa Wakenya kuhusu njama ya kuuawa kwa Dkt Ruto.

“Lengo kuu linapasa kuwa kubaini ikiwa kweli kulikuwa na njama yoyote ya kumwangamiza Naibu Rais. Na ikiwa ni kweli, wahusika wakamatwe,” akasema Bi Waruguru jana akiongea mjini Nanyuki, kaunti ya Laikipia

Mnamo Alhamisi Bw Itumbi alifikishwa kortini kuhusiana na barua feki iliyodai kuwa kuna njama ya kumuua Dkt Ruto.

Mbunge wa Sirisia John Waluke naye alimtaka Naibu Rais kutotishwa na madai kuwa kuna mpango wa kumuua, akisema hautafanikiwa.

“Tunawataka Wakenya kukulinda na kumkemea yeyote anayedhani atakuangusha,” akasema Bw Waluke, ambaye alikuwa katika hafla moja na Dkt Ruto.

Mbunge wa Kiminini Didmus Barasa alisema kama wafuasi wa Naibu Rais wako tayari kukamatwa kwa kumuunga mkono, akisema kuna watu wanaotaka kumuangusha kiongozi huyo.

Maelezo zaidi na CHARLES WASONGA

  • Tags

You can share this post!

Akiona kufurahisha kipusa kwa ujira wa watu

Malkia yatua nchini Misri kwa mpepetano wa Bara Afrika

adminleo