Habari MsetoSiasa

TANZIA: Ndingi Mwana'a Nzeki alikuwa mtetezi wa wanyonge

March 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

ASKOFU Mkuu mstaafu wa dayosisi ya Nairobi ya Kanisa Katoliki Ndingi Mwana’a Nzeki aliyefariki Jumanne akiwa na umri wa miaka 88, atakumbukwa kwa mchango wake katika elimu na kupigania demokrasia kwa kukosoa serikali ya Kanu.

Ndingi alifariki jana asubuhi katika makao ya viongozi wastaafu wa kanisa Katoliki jijini Nairobi baada ya kuugua kwa muda mrefu. Kifo chake kilitangazwa na kiongozi wa kanisa Katoliki nchini Kadinali John Njue.

“Ni asubuni yenye huzuni ambapo Askofu Mkuu Kadinali John Njue anatangaza kifo cha Askofu mkuu mstaafu wa Nairobi Ndingi Mwana’a Nzeki aliyefariki katika makao ya viongozi wa kidini Nairobi akiwa na umri wa miaka 88,” ilisema taarifa kutoka dayosisi ya Nairobi.

Kwenye ujumbe wake wa rambirambi Rais Uhuru Kenyatta alisema Ndingi atakumbukwa kama kiongozi shupavu wa kidini aliyejawa na upendo.

Wengine waliotuma risala zao za rambirambi wakimsifu marehemu kama mpiganiaji wa haki, ni Naibu Rais William Ruto, Kiongozi wa ODM Raila Odinga, Jaji Mkuu David Maraga, Gavana wa Mombasa Hassan Joho miongoni mwa wengine.

Kabla ya kuteuliwa Askofu Mkuu wa dayosisi ya Nairobi, Ndingi alihudumu kwa miaka mingi dayosisi ya Nakuru katika wadhifa huo.

Alizaliwa 1931, Mwala kaunti ya Machakos na baada ya kukamilisha masomo ya shule ya msingi alijiunga na mafunzo ya upadre katika seminari moja eneo la Kiserian, kaunti ya Kajiado.

Hata baada ya kutawazwa padri mwaka wa 1961, alisoma binafsi na kufaulu hadi akasomea digrii katika theolojia na usimamizi.

Kabla ya kuteuliwa Askofu, alihudumu kama padri katika parokia ya Makadara, Nairobi.

Kulingana na taarifa kutoka afisi ya mawasiliano ya dayosisi ya Nairobi, Ndingi alihudumu kama Askofu wa dayosisi ya Machakos kati ya 1969 na 1971 alipohamishwa kusimamia dayosisi ya Nakuru.

Akiwa Nakuru, alipata sifa kwa kutetea wanyonge hasa wakati wa vita vya kikabila vya 1992 eneo la Molo.

Ndingi alihatarisha maisha yake kwa kuhifadhi waliofukuzwa makwao katika makao yake.

Alilaumu watu waliokuwa na ushawishi katika serikali ya Kanu kwa kuchochea mapigano ya kikabila eneo la Rift Valley.

Mwaka wa 1996 alihamishwa hadi Nairobi ambapo alisaidiana na aliyekuwa Kadinali Maurice Otunga na mwaka mmoja baadaye aliteuliwa kuwa mrithi wa Otunga kama Askofu Mkuu wa dayosisi ya Nairobi.

Ndingi ambaye hakuchelea kukosoa serikali ya Kanu kwa uongozi mbaya hadi alipostaafu mwaka wa 2007 akiwa na umri wa miaka 75.

Mrithi wake, Kadinali John Njue alikuwa msaidizi wake alipokuwa Askofu Mkuu wa dayosisi ya Nakuru. Alikohudumu, alisaidia kujenga taasisi za elimu ikiwa ni shule na vituo vya mafunzo.

Katika kaunti ya Machakos moja ya shule alizoanzisha imepatiwa jina lake. Jana, viongozi wa kanisa Katoliki nchini waliongoza wanasiasa na waumini kumuomboleza.

Askofu Paul Kariuki wa dayosisi ya Embu aliomba Mungu aifariji familia yake na wote aliohudumia katika maisha yake kama kiongozi shupavu wa kanisa Katoliki.