Tanzia: ‘Tiktoker’ maarufu Brian Chira aaga dunia kufuatia ajali
NA WANDERI KAMAU
MSANII Brian Chira, mtumiaji maarufu wa mtandao wa Tiktok kufikisha ujumbe kwa mashabiki wake, ameaga dunia.
Kulingana na polisi, barobaro huyo aliaga dunia kufuatia ajali ya barabarani iliyofanyika Ijumaa usiku katika eneo la Karuri, Kaunti ya Kiambu.
Polisi walisema kuwa mwili wake ulichukuliwa kutoka eneo la ajali Jumamosi asubuhi na kupelekwa katika mochari ya City, jijini Nairobi.
Kulingana na ripoti za polisi, marehemu aligongwa na gari lililokuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi, ijapokuwa hawakutoa taarifa zaidi.
Mwili wake ulipelekwa katika mochari hiyo mwendo wa saa tisa alfajiri. Mwili huo ulikuwa na majeraha mabaya kichwani.
Polisi pia walisema kuwa kabla ya ajali hiyo, marehemu alikuwa ameenda kubugia mvinyo katika baa moja eneo la Gacharage, ambapo alizua vurugu. Kutokana na hilo, alifurushwa nje ya baa hiyo.
Baadaye, alichukua pikipiki kuelekea nyumbani kwao. Alishuka kutoka pikipiki hiyo na kujaribu kuvuka barabara kwa miguu.
Marehemu aligongwa na lori lililokuwa likisafiri kwa mwendo wa kasi, ijapokuwa halikusimama. Polisi walisema kuwa tukio hilo linaendelea kuchunguzwa.
Mmoja wa jamaa zake waliokuwa kwenye mochari hiyo kuutazama mwili huo alithibitisha kifo chake.
“Ni kweli. Ametuacha,” akasema bila kutoa maelezo zaidi.
Habari za kifo chake zilisambaa kote katika mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wake walichukulia habari hizo kama ‘kiki’, ikizingatiwa barobaro huyo alikuwa na mazoea ya kuzua ubishi mitandaoni.
Alikuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kabarak, alikokuwa akisomea masuala ya uchumi.