'Tiger Power' amiminiwa sifa katika mazishi yake
Na GEORGE MUNENE
HUZUNI ilitanda wakati mwanamume anayeaminika kuwa na nguvu zaidi Kenya, Bw Conrad Njeru Karukenya, almaarufu Tiger Power alipozikwa katika kijiji cha Makuria, Kaunti ya Embu.
Waombolezaji walibubujikwa machozi wakati jeneza lake liliposhushwa kaburini.
Mamia ya waombolezaji kutoka pembe tofauti za Kenya walijitokeza kumpa buriano mwanamume huyo aliyeweka historia kwa kuibuka mshindi katika kila shindano la kupima nguvu aliloshiriki humu nchini.
Wakati mmoja marehemu aliorodheshwa wa pili mwenye nguvu zaidi ulimwenguni kwenye shindano lililofanywa Uingereza.
Waliohudhuria mazishi yake walimsifu Bw Karukenya kama shujaa ambaye sifa zake zilienea kwa kasi.
“Alikuwa mwanamume mnyenyekevu na mwenye nguvu sana ambaye nguvu zake hazikumithilika Kenya,” akasema Gavana wa Kaunti ya Embu, Bw Martin Wambora.
Gavana huyo alisema Bw Karukenya alikuwa rafiki wa karibu wa familia yake na pia mshauri wa kisiasa.
“Wakati nilipokuwa nawania ubunge katika eneobunge la Runyenjes, Bw Karukenya alikuwa mshauri wangu kando na kusimamia kikosi changu cha usalama. Kutokana na ushauri wake, nilishinda kiti hicho kwa idadi kubwa mno ya kura,” akasema Bw Wambora.
Aliongeza kuwa eneo hilo na nchi nzima imepoteza mwanamume mwema ambaye sifa zake zitasalia akilini mwa wengi daima.
Awali, makasisi wa Kanisa Katoliki waliokuwa wamevaa kanzu nyeupe walifanya misa ya wafu ya kuvutia katika Shule ya Upili ya St Paul’a Kevote wakamsifu marehemu kama mwanamume ambaye alibatizwa katika imani ya kanisa hilo na anayefaa kuigwa na vijana.
Mbunge Maalumu, Bi Cecily Mbarire alisema alimfahamu Bw Karukenya wakati alipokuwa msichana mdogo wa shule.
“Wakati mmoja nilishtuka nilipomwona Karukenya akiruhusu gari aina ya Land Rover limkanyage na hakujeruhiwa hata kidogo,” akasema Bi Mbarire, akaongeza kuwa marehemu alifahamika na wengi na aliyeletea Kaunti ya Embu sifa tele.
Spika wa Bunge la Kaunti ya Embu, Bw Steve Simba alimwomboleza marehemu kama mtu asiye na ubinafsi na mwenye bidii ambaye tabia zake zilikuwa njema.
Aliongeza pia kuwa alikuwa mwaminifu na viongozi wanafaa kumwiga.
“Jina lake Conrad linamaanisha uaminifu na Bw Karukenya hakusaliti jina lake kwani hakuwa fisadi na viongozi wanafaa kumwiga,” akasema Bw Simba ambaye pia ni diwani wa wadi ya Runyenjes ya Kati.