'Total Man' alitenga Sh10 milioni kulinda kaburi lake
Na GEOFFREY ANENE
“Total Man” Nicholas Biwott alitenga Sh10 milioni za kuhakikisha kaburi lake linalindwa vyema katika maagizo kuhusu jinsi mali yake itagawanywa, gazeti la humu nchini limeripoti.
Waziri huyu wa zamani katika Serikali ya Rais Daniel arap Moi, ambaye ni bilionea, aliaga duniani akiwa na umri wa miaka 77 kutokana na matatizo ya figo mnami Julai 11 mwaka 2017. Gazeti hilo la Kenya limesema kwamba matakwa yamesomwa na kufichua vitu vya kustaajabisha.
Mwendazake Biwott alitenga fedha hizo kwa matumizi ya kulinda kaburi lake na la babake Kiprono Cheserem katika kijiji cha Toot katika kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Mbali na mamilioni hayo ya kuhakikisha makaburi hayo yanaangaliwa vyema, Biwott alitambua bibi yake mmoja katika stakabadhi hiyo, ingawa alikuwa nao wanne.
Kulingana na matakwa ya marehemu Biwott, washirika wake watapata mali yote na biashara walizomiliki naye kwa pamoja, gazeti hilo limesema.