Habari Mseto

Tulipigwa na polisi tukiwa seli, wakimbizi waambia mahakama

May 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

Wakimbizi 20 waliokamatwa Ijumaa nje ya ofisi ya Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) jijini Nairobi, Jumatatu walieleza mahakama walivyoteswa wakiwa seli za polisi.

Wakimbizi hao wakiwemo wanawake wawili na mvulana mwenye umri wa miaka 14, waliambia mahakama kwamba polisi waliwatesa sana wakiwa katika seli za kituo cha polisi cha Kileleshwa ikiwa ni pamoja na kulala wakiwa wamefungwa kwa nyororo.

“Haki zetu zilikiukwa. Tulipigwa kama wanyama tangu Ijumaa na kunyimwa matibabu. Hatukuruhusiwa kuwasiliana na jamaa na mawakili wetu,” alisema Lumumba James akitokwa na machozi.

Walitoa kilio hicho baada ya upande wa mashtaka kuomba wasisomewe mashtaka hadi Jumanne akisema polisi walitaka kuwaongezea mashtaka zaidi.

“Nimearifiwa na polisi kwamba wanapanga kuwaongezea washukiwa mashtaka zaidi. Wanaomba wazuiliwe rumande katika Gereza la Viwandani hadi kesho watakaposomewa mashtaka,” alisema kiongozi wa mashtaka.

Wakimbizi hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Kibera Boaz Ombewa na polisi walikuwa wameandaa mashtaka ya kuzua ghasia na kuvuruga amani nje ya ofisi za UNCHR mtaani Westlands, Nairobi, kuandaa mkutano haramu, kuchochea umma kushambulia walinzi wa kampuni ya G4S na maafisa wa polisi waliokuwa wakilinda ofisi hizo na kujaribu kuokoa baadhi yao waliokuwa wamekamatwa na polisi.

Bw Ombewa aliwafahamisha kwamba mashtaka mengine dhidi yao ni kushambulia maafisa wa polisi waliokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kudumisha amani. “Nimewafahamisha tu mashtaka ambayo polisi walikuwa wameandaa lakini hamtajibu kwa sababu wameomba mahakama iahirishe hadi kesho,” alisema Bw Ombewa.

Washukiwa hao walidai kwamba hawakuwa wamefahamishwa sababu za kukamatwa kwao tangu Ijumaa. “ Walichofanya maafisa wa polisi ni kutupiga na kututesa tukiwa seli,” walisema na kuomba waachiliwe ili wakapate matibabu.

Hata hivyo, Bw Ombewa aliwafahamisha kwamba kwa sababu polisi waliomba muda wa kuongeza mashtaka zaidi, hangeweza kuwaachilia.

“Wale ambao mna zaidi ya umri wa miaka 18 mtazuiliwa katika gereza la viwandani hadi Jumanne na nimeagiza mpelekwe kutibiwa. Mvulana aliye na umri wa miaka 14 atazuiliwa katika gereza la watoto na wanawake watazuiliwa katika gereza la wanawake la Langata,” Bw Ombewa aliamua.