Tumbojoto mawaziri wakirejea kazini
Na DAVID MWERE
MAWAZIRI waliopewa likizo ya Krismasi mnamo Desemba 21, 2018 wanatarajiwa kurejea kazini siku ya Jumatatu huku uvumi ukienea kwamba huenda Rais Uhuru Kenyatta akawapiga kalamu baadhi yao kutokana na utendakazi duni.
Kwenye taarifa iliyotumwa kwa mawaziri, makatibu wa wizara na Mwanasheria Mkuu mnamo Desemba 18 mwaka jana, Rais aliwataka wateue maafisa watakaosimamia shughuli katika wizara zao kwa muda ambao wangekuwa likizoni.
Hata hivyo, kurejea kwao afisini kumegubikwa na minong’ono kwamba huenda Rais Kenyatta akafanya mabadiliko makubwa katika serikali yake miezi 10 baada ya kuridhiana na kiongozi wa upinzani, NASA, Raila Odinga na kuzika tofauti zao waliposhindania urais katika uchaguzi mkuu wa 2017.
Kulingana na Bw Barasa Nyukuri ambaye ni mataalamu wa masuala ya uongozi, mabadiliko katika baraza la mawaziri yatatekelezwa hivi “karibuni”.
“Mabadiliko hayo yalipasa kutekelezwa siku chache baada ya Rais kuridhiana na Bw Odinga, lakini yalicheleweshwa kutoa nafasi kwa mashauriano zaidi”, akasema Bw Nyukuri.
Ubashiri
Mtaalamu huyu anabashiri kuwa katika mabadiliko hayo, huenda watu wapya wakateuliwa katika baraza la mawaziri kwa ajili ya kumsaidia Rais kutekeleza Agenda zake Nne Kuu za Maendeleo.
“Ipo haja kubwa ya mabadiliko serikalini. Baadhi ya watu ambao Rais anafanya kazi nao wameonyesha wazi kuwa hawajahitimu kutoa huduma kwa wananchi huku baadhi yao wakihusishwa katika kashfa za ufisadi” Bw Nyukuri akaongeza.
Mnamo Alhamisi jioni Bw Odinga alisafiri hadi Mombasa ambapo jana alipangiwa kukutana na Rais katika Ikulu. Japo, yale ambayo viongozi hao alizunguzia hayakujulikana, mwandani mmoja wa Rais alidokezea Taifa Leo kwamba, mazungumzo hayo yalihusu mabadiliko serikalini.