Tunalazimishwa na serikali kununua mahindi ya sumu – Kampuni
Na BARNABAS BII
BODI ya kusimamia Hifadhi ya Chakula (SFR) na Bodi ya Nafaka na Mazao nchini (NCPB) zimejipata pabaya kufuatia madai kuwa ziliruhusu usambazaji wa mahindi yenye sumu ya aflatoxin ambayo husababisha kansa.
Kampuni za kusaga unga wa mahindi Jumapili zilidai kuwa bodi ya SFR imekuwa ikizitaka zinunue mahindi yaliyo na sumu ya aflatoxin na wachanganye na mahindi safi kwa lengo la kuzuia uhaba wa chakula nchini.
“Tumekuwa tukikwepa kununua mahindi ya NCPB yaliyovunwa 2018/2019 hasa katika maghala yaliyoko Bungoma, Kisumu na Nakuru kwa sababu yana sumu ya aflatoxin.
“Lakini bodi ya SRF inasisitiza kwamba tununue mahindi hayo yenye sumu na kisha tuchanganye na mahindi safi,” akasema afisa wa kampuni moja ya kusaga unga wa mahindi aliyeomba jina lake libanwe kutokana na hofu ya kuandamwa na serikali.
Lakini mwenyekiti wa bodi ya SFR Dkt Noah Wekesa, alipuuzilia mbali madai hayo kwa kusema mahindi machafu ni chakula cha mifugo na wala hayafai kutumiwa na binadamu.
Alisisitiza kuwa kuchanganya mahindi yasiyofaa kuliwa na binadamu na mahindi safi ni kinyume cha sheria.
“Mahindi ya gredi 1 ndiyo salama kwa afya ya binadamu. Lakini mahindi ya gredi 4 yanafaa kutengenezwa chakula cha mifugo. Inashangaza kwamba wasagaji wa unga wanadai kuwa wanalazimishwa kuchanganya unga wa mahindi ya gredi 1 na gredi 4,” Dkt Wekesa akaambia Taifa Leo katika mahojiano kwa njia ya simu.
Kuna jumla ya magunia 100,000 ya mahindi ya gredi 4 katika maghala ya NCPB, hasa katika maeneo ya Magharibi mwa Kenya.
Kulingana na kampuni za kusaga unga, mahindi ya gredi 4 yanasadikiwa kuwa na sumu ya aflatoxin na yanaaminika yaliingizwa humu nchini na wafanyabiashara walaghai kutoka Uganda.
Wafanyabiashara hao wanadaiwa kununua mahindi hayo kwa Sh1,600 kwa kila gunia na kuuzia bodi ya NCPB kwa Sh3,200 kwa gunia.
Shirika la Kutathmini Ubora wa Bidhaa (Kebs) hivi karibuni lilipiga marufuku unga wa Dola na Tetema kwa kushindwa kuzingatia ubora na kuuza unga unaodhuru afya.
Serikali ya Kaunti ya Kiambu imeagiza idara ya afya kuchunguza unga wa Soko ambao pia leseni yake ilisitishwa kutokana na hofu ya kuwa na sumu aflatoxin.