Tunatambua Kalonzo pekee, Kibwana aambiwa
BENSON MATHEKA na CHARLES WASONGA
VIONGOZI wa Ukambani wamemshambulia Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana na kukariri kuwa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka bado ndiye kigogo wa kisiasa eneo hilo.
Wakiongea katika sherehe ya kutoa shukrani iliyoandaliwa na Mbunge wa Kathiani, Robert Mbui, katika Shule ya Msingi ya Mbuuni, viongozi hao wakiwemo wabunge 16 waliwapuuzilia mbali wale wanaodai kuwa Bw Musyoka amepoteza umaarufu eneo hilo.
Viongozi hao walisema wenye fikra kama hizo ni watu waliopoteza mwelekeo na ambao hawaheshimiwi na wakazi wa eneo hilo. Bw Mbui, ambaye ni Naibu Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa na wabunge wenzake walisema wanamtambua Bw Kalonzo kama mgombeaji urais wa kipekee kutoka jamii yao kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
Bw Musyoka amekuwa akipingwa na magavana wa eneo hilo Alfred Mutua (Machakos) Charity Ngilu (Kitui) na Kivutha Kibwana (Makueni) wanaomtaka astaafu siasa na kusahau urais.
Wabunge wengine kutoka Ukambani waliohudhuria sherehe hiyo ni pamoja na Makali Mulu (Kitui ya Kati), Gideon Mulyungi (Mwingi ya Kati), Patrick Makau (Mavoko), Charles Nguna (Mwingi Magharibi) na Joshua Kimilu (Kaiti).
Wengine walikuwa Julius Mawathe (Embakasi Kusini), Nimrod Mbai (Kitui Mashariki), Evanson Kivasu (Mbooni) na William Kamket (Tiaty, Kanu) na Anthony Oluoch (Mathare, ODM).
Wabunge hao walimshambulia Gavana Kibwana ambaye majuzi alinukuliwa katika vyombo vya habari akimtaka Bw Musyoka kustaafu kutoka siasa.
“Tunamwonya Gavana Kibwana kukoma kumdunisha Kalonzo. Huyu ni mtu ambaye anataka kumharibia kiongozi wetu baada ya kung’amua kuwa hana ufuasi wowote wa haja hapa Ukambani,” akasema Bw Mbui.
Bw Mulu alimtaja Makamu huyo wa Rais wa zamani kama kiongozi mwenye ufuasi katika pembe zote nchini.
Bw Kimilu alisema wananchi wote wa kaunti ya Makueni wako nyuma ya Musyoka.
“Sisi kama watu wa Makueni tunamuunga mkono Kalonzo pamoja na ndoto yake ya kuwa rais wa Kenya mnamo mwaka wa 2022. Profesa Kibwana hana ushawishi wowote baada ya kujiondoa kutoka Wiper,” akaeleza.
Bw Oluoch alimpongeza Bw Musyoka kwa kusimama na Bw Odinga katika chaguzi zilizopita na hatua yake ya kuunga mkono handisheki.
Naye Bw Kamket aliwasilisha salamu kutoka kwa Seneta Moi huku akitoa wito kwa jamii ya Wakamba kudumisha umoja wao.