Habari Mseto

Tusaidieni kuwatambua wanaokeketa wasichana kisiri – Serikali

November 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ONDIEKI

[email protected]

Huku vita dhidi ya ukeketaji wa wasichana vikiendelea humu nchini, wakazi wa Kaunti ya Nakuru Jumatatu wameshauriwa kushirikana na vyombo vya usalama ili kusaidia kumaliza uovu huo.

Kamanda wa polisi katika kaunti ya Nakuru Bw Stephen Matu alisema ukeketaji wa wasichana unaendeshwa kisiri vijijini bila ufahamu wa wengi, na hufanyiwa wasichana wadogo wasiokuwa na uwezo wa kujitetea.

Kaunti ya Nakuru imetambuliwa kuwa mojawapo ya kaunti ambazo bado zinafanya mila hiyo.

Mkuu huyo wa polisi alisisitiza kuwa shuguli hiyo ni kinyume cha sheria na kuwa mila ambayo imepitwa na wakati. “Nataka kuonya wale ambao wanafikiria kufanya shughuli hiyo kuwa watakumbana na sheria kali,” alisema Bw Matu.

Alitaja ukeketaji kuwa ubaguzi kwa jinsia ya kike na ambao sio tu unadhalilisha haki yao, bali pia usalama wao na afya.

“Shughuli ya ukeketaji haina nafasi tena karne hii ya ishirini na moja,” aliongeza. Bw Matu alitoa wito kwa viongozi, walimu na wazazi mjini Nakuru kuungana na kuripoti visa vya ukeketaji kwa vyombo vya usalama.

“Naomba wakazi hasa wa kaunti hii ya Nakuru kuungana na katika vita dhidi ya ukeketaji kwa sababu ni ukiukaji wa haki za kibinadamu,” alisema.

Aliongeza kuwa wameweka mikakati ya kutosha kuhakikisha usalama wakati wa likizo ndefu ya wanafunzi. Maafisa wa usalama kutoka ngazi zote ikiwemo machifu na manaibu wao wamehamasishwa kuwa macho usiku na mchana ili kuzuia uovu huo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, polisi mjini Nakuru walikamata mwanamke ambaye wanawe wawili wa kike walikeketwa kwa njia ya kutatanisha. Mwanamke huyo alipelekwa katika mahakama mjini Nakuru na ambapo alishtakiwa kwa kufanikisha shughuli ya ukeketaji kinyume cha sheria, na kuachiliwa kwa dhamana.

Watoto hao wawili wanaendelea kupata nafuu katika hospitali kuu ya Nakuru Level 5, baada ya kuokolewa na maafisa wa usalama kutoka kituo cha polisi cha Elementaita. Mmoja wa wauguzi kutoka hospitali hiyo alisema kuwa wawili hao walikatwa vibaya.