Tuzo ya Safal-Cornell: Kuna haja kwa Wakenya ‘kukutana nyuma ya hema’
NA PROF IRIBE MWANGI
TUZO ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika: Nilipoandika jina la tuzo hii sikulipenda, niliona kuwa lina “ya” nyingi mno, lakini si neno, tuzo inaeleweka!
Ni tuzo muhimu ya Kiswahili inayofadhiliwa na Kampuni ya Safal, Chuo Kikuu cha Cornell na Wakfu wa Ngugi wa Thiong’o kati ya wengine.
Tuzo hii iliasisiwa mnamo 2014 na madaktari Lizzy Attree na Mukoma wa Ngugi. Mwezi uliopita niliandika kuhusu umuhimu wa tuzo za uandishi.
Nafurahi kuwa uandishi wa Kiswahili unazidi kuthaminiwa kunapokuwa na zawadi ya Dola 15,000 (takribani shilingi milioni mbili na nusu za Kenya).
Tuzo ilitolewa tarehe 9 mwezi huu katika hoteli moja jijini Nairobi.
Wageni wengi walihudhuria hafla hiyo: maprofesa wa Kiswahili, wanahabari, waandishi, wanafunzi, wafanyabiashara, wanasiasa na wakereketwa wa Kiswahili.
Mgeni rasmi alikuwa Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki Dkt Caroline Asiimwe.
Jaji Mkuu alikuwa ni Prof K.W. Wamitila wa Chuo Kikuu cha Nairobi na alisaidiana na Dkt Zuhura Badru wa Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na Ali Rashid wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Mwaka huu, washindi wote walitoka Tanzania. Philipo Oyaro ndiye aliyekuwa mshindi wa bunilizi akifuatiwa na Ahmad Simba.
Fatuma Salim alishinda utunzi wa mashairi akifuatiwa na Lenard Mtesigwa. Kila mshindi wa kwanza alipata Dola 5,000 naye wa pili akapata Dola 2,500.
Hali ilikuwa vivyo hivyo mnamo 2017 japo majaji wote watatu (marehemu Ken Walibora, Dkt Richard Wafula na mimi) walitoka Kenya.
Kuna haja ya waandishi kutoka Kenya “kukutana nyuma ya hema.”