Habari Mseto

Uavyaji mimba utasalia kuwa hatia – Mahakama

June 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JUMA NAMLOLA

MAHAKAMA Kuu Jumatano ilikataa mbali ombi la kutaka utoaji mimba kuwa halali, ikisema kitendo hicho kitaendelea kuwa haramu kwa mujibu wa Katiba.

Majaji watano walitupilia mbali ombi la Shirikisho la Mawakili Wanawake (FIDA), Kituo cha haki za Uzazi (Centre for Reproductive Rights) na wadau wengine kwamba mahakama ilegeze kamba na kuwaruhusu wajawazito kuavya mimba kwa njia salama.

Wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo, mtaalamu wa uzazi Profesa Joseph Kamau alikuwa amewaeleza majaji Aggrey Muchelule, John Mativo, George Odunga, Lydia Achode na Mumbi Ngugi kuwa mtoto ambaye hajazaliwa si binadamu, na kwamba hana haki ya kuishi.

Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu alikuwa ameeleza kuwa kuna nyakati ambapo maisha ya mama huwa hatarini, lakini hakuna mwongozo kuhusu hatua ya kuchukuliwa bila ya daktari au mkunga kuvunja sheria.

Walalamishi walikuwa wamedai wanawake wanapopata mimba kwa njia ambazo hawatarajii huavya mimba vichochoroni.