Uber mbioni kujitosa kwa uchukuzi wa umma
Na BERNARDINE MUTANU
Kampuni ya uchukuzi ya Uber inalenga kuanzisha apu mpya ili kuwasaidia abiria wanaotaka kuhifadhiwa viti ndani ya magari ya uchukuzi wa umma.
Ikiwa majaribio yanayofanywa Misri na Mexico yatafaulu, huenda teknolojia hiyo ikazinduliwa humu nchini kulingana na afisa wa kampuni hiyo.
Uber inakadiria kuwa zaidi ya thuluthi moja ya Wakenya Jijini hutumia magari ya umma.
“Tunataka kuwa sehemu ya mfumo wa uchukuzi Nairobi na matatu ni njia muhimu sana ya uchukuzi wa umma,” alisema, na meneja wa Uber wa Afrika Mashariki Loic Amado.
Tayari, kampuni hiyo ilianzisha apu ya uchukuzi wa umma, Uber Pool na Uber Express katika miji kama vile London na New York.
Apu hizo huwawezesha watu wanaoelekea upande mmoja kuchukua gari moja.
Uber ilianzisha huduma zake Kenya miaka minne iliyopita na kufikia sasa ina madereva 6,000.