Habari MsetoSiasa

Uchaguzi: ODM na Wiper tayari kumenyana Embakasi

April 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

RUSHDIE OUDIA na WANDERI KAMAU

WAPIGAKURA katika maeneobunge ya Embakasi Kusini na Ugenya watawachagua wabunge wapya Ijumaa kwenye chaguzi ndogo wanazotarajiwa kushiriki baada ya muda wa kampeni kuisha rasmi mnamo Jumanne.

Katika eneobunge la Embakasi Kusini, kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa Ford-Kenya, Moses Wetang’ula walitumia muda wao kumfanyia kampeni za nyumba hadi nyumba, Bw Julus Mawathe, anayewania kwa tiketi ya Wiper.

Bw Mawathe ndiye alikuwa mbunge wa eneo hilo, kabla ya mahakama kufutilia mbali kuchaguliwa kwake, kufuatia kesi iliyowasilishwa na mtangulizi wake, Bw Irshad Sumra.

Mwaniaji huyo anawania kwa tiketi ya chama cha ODM. Bw Kalonzo alieleza imani yake kwamba Bw Mawathe ataibuka mshindi.

Uchaguzi huo unaonekana kuwa ushindani wa ubabe wa kisiasa kati ya ODM na Wiper.

Kwenye kampeni zake, viongozi wa ODM wamekuwa wakiwarai wapigakura kumchagua Bw Sumra, kwani “alinyang’anywa” kiti hicho, kulingana na uamuzi wa mahakama kufutilia mbali uchaguzi wa Bw Mawathe.

Kampeni za ODM zimekuwa zikiongozwa na Katibu Mkuu, Bw Edwin Sifuna na mbunge wa Makadara, Bw George Aladwa.

Katika eneobunge la Ugenya, wawaniaji wawili wanashinikiza kuondolewa kwa wenzao wawili kwa madai ya kukiuka kanuni za kampeni zilizowekwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Mnamo Jumanne, wawaniaji hao walizuru sehemu mbalimbali za eneobunge hilo, wakiwarai wakazi kuwapigia kura.

Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi katika eneobunge hilo, Bw Vincent Saitabau, jana alisema kwamba wamejitayarisha kikamilifu kuendesha uchaguzi huo, kwani maafisa wote watakaohusika wamepewa mafunzo ya kutosha.

Vile vile, alisema kuwa vifaa vyote vya uchaguzi vimo tayari. Uchaguzi huo utaendeshwa katika vituo 112.

Hata hivyo, wawaniaji Brian Omondi wa Thirdway Alliance na Daniel Juma wa chama cha Grand Dreams Party walilalama kwamba wenzao wa ODM na chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG) walikiuka sheria za kampeni kwa kupitisha muda uliowekwa.

Mwaniaji wa ODM ni David Ochieng’ naye wa MDG ni Christopher Karani.

Wawili hao pia walilalama kuwa wawaniaji hao wamekuwa wakizua ghasia kwenye kampeni zao.

Tayari, Bw Omondi ameiandikia barua IEBC hofu yao kuhusu wawili hao kushiriki katika uchaguzi huo, akisema hawafai.