• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Uchaguzi wa kupata viongozi wa GTMA wasababisha zogo

Uchaguzi wa kupata viongozi wa GTMA wasababisha zogo

Na SAMMY WAWERU

UCHAGUZI wa kupata viongozi wapya wa muungano wa wahudumu wa tuktuk Githurai 45 na magari madogo ya usafiri na uchukuzi – GTMA – uliofanyika Novemba umeibua zogo.

Baadhi ya wawaniaji wa nyadhifa za uongozi kwenye uchaguzi huo uliofanyika mnamo Novemba 13, 2020, wameeleza kutokuwa na imani na matokeo.

Malalamishi hayo yameibuka licha ya zoezi hilo linalofanyika kila baada ya miaka miwili (ingawa awali lilikuwa kila baada ya mwaka mmoja, Katiba ya GTMA ilipofanyiwa marekebisho ikapendekwa uchaguzi uwe kila baada ya miaka miwili), kusimamiwa na serikali, chini ya afisi ya Masuala ya Jinsia, Utamaduni na Huduma za Kijamii (SCDO), Kaunti ndogo ya Ruiru.

Githurai 45, ipo katika eneobunge la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Baadhi ya wagombea wa kiti cha mwenyekiti, na kilichokuwa na wawaniaji watatu, wamepinga uhalisia wa matokeo, wakihoji shughuli za kupiga kura na kuzihesabu zilisheheni utapeli.

Bw Peter Kinyua, na ambaye anatetea kuhifadhi kiti chake baada ya kuchaguliwa awamu ya kwanza Februari 2019 kama mwenyekiti, katika uchaguzi wa mwaka huu, 2020 aliibuka kidedea.

Matokeo yaliyotangazwa, yalionyesha anafuatwa na mpinzani wake Laban Wamae (ambaye amehudumu kama naibu mwenyekiti tangu 2019). Mgombea mwingine wa kiti hicho anatambulika kama Sammy, na ambaye amewahi kuwa mwenyekiti.

 

Baadhi ya wanachama wa muungano wa tuktuk na magari madogo Githurai – GTMA – wakati wa uchaguzi mwezi Novemba 2020. Picha/ Sammy Waweru

Nyadhifa zingine ambazo matokeo ya kura yamepingwa ni pamoja na kile cha karani na naibu wa karani, kati ya nyinginezo.

Mapema juma hili, SCDO iliandikia GTMA barua ikitaka kukutana na wagombea wote. “Mkutano huo utahusisha wagombea wote,” inaeleza barua hiyo.

Uchaguzi wa muungano huo 2020 ulifanyika katika ukumbi wa mikutano, ulioko katika afisi ya D.O, Githurai, chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa polisi.

Aidha, ulikuwa na jumla ya nyadhifa tisa zilizowaniwa, chini ya usimamizi wa tume ya muda, shughuli hiyo ikiiga nyayo za tume huru ya uchgauzi na uratibu wa mipaka (IEBC), katika kuendesha uchaguzi.

Kila mgombea alikuwa na ajenti wake, SCDO ikisisitiza haja ya kutii sheria zilizowekwa kusaidia kuzuia msambao wa Covid-19 wakati wa upigaji kura.

Kulingana na baadhi ya wanachama wa GTMA, uchaguzi wa Februari 2019, ulikuwa wenye amani na uliopigiwa upatu, kwa kuipa IEBC namna ya kutekeleza uchaguzi huru, haki na wenye uwazi.

GTMA ina zaidi ya tuktuk na magari madogo 300.

You can share this post!

Wakenya asilimia 67 wanaamini ufisadi umeongezeka nchini...

Nondies wajinasia huduma za wanaraga watano matata