Uchunguzi wa majaji 13 watishia kulemaza korti
Na RICHARD MUNGUTI
MAJAJI 13 wa Mahakama ya Juu na Mahakama Kuu wanachunguzwa kwa madai ya kushiriki ufisadi na ukiukaji wa maadili ya kazi.
Kesi dhidi ya majaji hao zinaendelea kusikizwa na majopo mawili ya Tume ya Kuajiri Watumishi katika Idara ya Mahakama (JSC). Majopo hayo yanaendelea kupokea ushahidi dhidi ya majaji hao katika Mahakama ya Juu na Jengo la Kenya-Re jijini Nairobi.
Majaji walioshtakiwa kwa JSC wanajumuisha majaji watano wa Mahakama ya Juu na majaji wanane wa Mahakama Kuu.
Wanaoshtakiwa ni pamoja na Jaji Mkuu (CJ) David Maraga , Jaji Mohammed Ibrahim, Jaji Smokin Wanjala , Jaji Njoki Ndung’u na Jaji Jackton Ojwang ambaye wiki iliyopita alisimamishwa kazi na Rais Uhuru Kenyatta.
Mwingine aliyewatangulia hao ni naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu.
Kusimamishwa kazi kwa Jaji Ojwang kumeyumbisha utenda kazi katika mahakama hiyo ya upeo.
JSC na Mahakama kuu ikiamua kesi ya ufisadi dhidi ya Jaji Mwilu iendelee, basi mahakama hiyo itakuwa imesalia na Jaji mmoja tu- Jaji Isaack Lenaola ambaye hajalimbikiziwa lawama.
Jaji Mwilu alikoma kufanya kazi baada ya kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya ufisadi mbele ya hakimu mkuu Lawrence Mugambi Agosti mwaka uliopita.
Rais Kenyatta aliteua jopo lenye wanachama watano kuamua hatma ya Jaji Ojwang.
Mwenyekiti wa jopo hilo ni Jaji Alnashir Visram wa Mahakama ya Rufaa.
Kurunzi ya kumulika ufisadi katika idara ya mahakama ilimwangazia Jaji Mwilu aliyekamatwa na kushtakiwa Agosti mwaka uliopita.
Jaji Enock Mwita wa Mahakama alisitisha kusikizwa kwa kesi na uamuzi utatolewa Mei 31,2019 na majaji watano walioteuliwa na Jaji Maraga..
Mashtaka dhidi ya CJ Maraga ni kuwa ni mbaguzi, mwenye ukabila na mkaidi wa maadili ya mahakama kwa kuhudhuria mikutano ya kisiasa Kisii na Nyamira.