Habari Mseto

Uchunguzi waanzishwa dhidi ya mshukiwa aliyeelekeza droni juu ya kituo cha polisi Lamu

December 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KALUME KAZUNGU

MAAFISA wa polisi, Kaunti ya Lamu wameanzisha uchunguzi dhidi ya mshukiwa aliyekamatwa kwa kupeperusha droni juu ya kituo cha Polisi cha Tchundwa, Lamu Mashariki.

Mshukiwa huyo ambaye ni raia wa Kenya alikamatwa Ijumaa majira ya saa moja unusu usiku baada ya kidege hicho kisichokuwa na rubani kuonekana kikipeperuka hewani kwenye kituo hicho cha polisi.

Kamanda wa Polisi wa Lamu, Moses Murithi alisema sababu ya mshukiwa huyo kutekelea kitendo hicho haijajulikana.

Alisema uchunguzi unaendelea na kwamba mshukiwa atapelekwa kortini kuanzia jumahili.

Bw Murithi aliwaonya wananchi dhidi ya kuendeleza tabia zenye kutiliwa shaka hasa kwenye vituo vya walinda usalama.

Alisisitiza kuwa vituo vya walinda usalama vimeorodheshwa kwenye gazeti rasmi la serikali kuwa maeneo yaliyoko chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa usalama na kwamba ni marufuku kwa vitendo vyoyote visivyoeleweka na ambavyo vinaonekana kuwa kero kwa usalama wan chi.

“Mshukiwa tulimkamata usiku wa Ijumaa baada ya kidege chake kisichokuwa na rubani kuonekana angani ndani ya kituo cha polisi cha Tchundwa. Kwa sabab bado anahojiwa ili kujua sababu zilizomfanya yeye kufanya hivyo. Tunamwasilisha kortini wakati wowote. Wananchi tungewasihi kuheshimu sheria na kuepuka kufanya vitendo visivyoeleweka karibu na vituo vya walinda usalama,” akasema Bw Murithi.

Raia mmoja aliyezungumza na Taifa Leo ameisifu hatua ya polisi ya kumtafuta na kumkamata aliyekuwa akielekeza kidege hicho kilichokuwa kikielea kwenye kituo cha polisi cha Tchundwa.

“Utaendeshaje roketi au droni ndani ya kituo cha polisi bila ruhusa. Bila shaka alikuwa na sababu za yeye kufanya hivyo. Apambane na hali yake,” akasema Bw Ahmed Salim.

Maeneo ya Tchundwa na Mbwajumwali yamekuwa yakigonga vichwa vya habari kila mara kutokana na mauaji ya kiholela ya machifu na walinda usalama.

Mnamo Juni 8, 2020, konstebo wa polisi, Rodgers Odhiambo ambaye alikuwa akihudumu kwenye kituo cha polisi cha Tchundwa aliuawa kwa kukatwakatwa kwa mapanga na watu wasiojulikana wakati akinunua bidhaa kwenye duka moja kijijini Tchundwa majira ya saa mbili usiku.

Oktoba 2019, konstebo mwingine wa polisi, Hesbon Okemwa Anunda, ambaye pia alikuwa akihudumu kwenye kituo cha polisi cha Tchundwa aliuawa kwa kukatwakatwa kwa mapanga na watu wasiojulikana na kisha mwili wake kutupwa kichakani kati ya Mbwajumwali na Kizingitini.

Desemba 11, 2019, machifu wawili, Mohamed Haji Famau na Malik Athman Shee waliuawa kwa kukatwakatwa kwa mapanga na watu wasiojulikana waliovamia ofisi yao kijijini Mbwajumwali majira ya saa sita adhuhuri.