• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
UDA sasa yaona heri ifanye uchaguzi kwa awamu kadhaa

UDA sasa yaona heri ifanye uchaguzi kwa awamu kadhaa

NA JUSTUS OCHIENG

CHAMA tawala cha Rais William Ruto, United Democratic Alliance (UDA) kitafanya uchaguzi katika awamu nne kuanzia Aprili 26 hadi Agosti 24 huku kikiunda vitengo vikuu mbalimbali kabla ya zoezi hilo.

Tangazo hilo limefuatia kikao cha Baraza Kuu ya Kitaifa kilichoongozwa na Dkt Ruto, ambaye ni kiongozi wa chama hicho, kilichofanyika jana katika makao makuu ya UDA jijini Nairobi.

“Kiongozi wa chama, Rais William Ruto, aliongoza mkutano wa Baraza kuu la Kitaifa (NSC) kwa niaba ya Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC). Mkutano wa NSC uliandaliwa kujadili uchaguzi wa chama hicho mashinani unaokaribia pamoja na katiba ya viungo mahsusi vya chama,” alisema Mwenyekiti wa Chama, Cecily Mbarire.

Alisema UDA imejitolea kuendesha uchaguzi huru na wa haki mashinani katika kaunti zote.

“Uchaguzi utafanyika kielektroniki katika awamu nne,” alitangaza.

Awamu ya kwanza itafanyika Aprili 26 na ambapo kaunti za Nairobi, Narok, Pokot Magharibi, Busia, Homa Bay, Isiolo na Garissa zitapiga kura.

Chama hicho kimetangaza kuwa awamu ya pili ya uchaguzi itafanyika Juni 22 katika kaunti za Mombasa, Uasin Gishu, Nyandarua, Tharaka Nithi, Machakos, Kisii, Bungoma, Siaya, Taita Taveta, Wajir, Tana River, Kwale na Marsabit.

Bi Mbarire alisema awamu ya tatu itafanyika Agosti 10 katika kaunti za Kiambu, Embu, Kericho, Meru, Migori, Kakamega, Nyamira, Kitui, Elgeyo Marakwet, Samburu, Kajiado, Mandera, Kilifi, Murang’a na Lamu.

Awamu ya nne inayopangiwa kufanyika Agosti 24 itaruhusu uchaguzi kufanyika katika kaunti za Nakuru, Bomet, Nyeri, Kirinyaga, Nandi, Baringo, Turkana, Laikipia, Trans-Nzoia, Kisumu, Vihiga na Makueni.

“Baada ya kukamilisha uchaguzi za mashinani katika kaunti zote, UDA itaendesha uchaguzi wa kaunti na kitaifa kufikia Disemba 2024,” alitangaza Bi Mbarire.

Alifichua kuwa NSC vilevile imeunda Bodi yake kusimamia Uchaguzi Nchini (NEB) yenye wanachama saba itakayoendesha uchaguzi na ambayo itaongozwa na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Kukusanya Ushuru (KRA), Anthony Mwaura kama mwenyekiti akishirikiana na naibu mwenyekiti, Veronica Kiberenge

Wanachama wengine wa NEB ni pamoja na: Lydia Munika, Jimmy Kaingi, Mary Mutinga, Halake Dida na Linda Kiome.

  • Tags

You can share this post!

Israel sasa yaondokea Hospitali ya Shifa ikiwa imeiharibu...

Afueni kwa wake wa pili wakipata idhini kuzika mume

T L