UFISADI: Kashfa mpya ya Sh1.7b yafichuka Wizara ya Michezo
Na DAVID MWERE
ZIMWI la Ufisadi linaloandama idara mbalimbali za serikali halijasaza Wizara ya Michezo baada ya afisi ya Mkaguzi Mkuu wa serikali kufichua sakata ya hivi punde ambapo Sh1.7b zilipotea katika wizara hiyo.
Pesa hizo ambazo haibaniki zilivyotumika ni sehemu ya Sh3.5 bilioni zilizotengewa Wizara ya Michezo wakati wa matayarisho ya Mashidano ya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 18 ulioandaliwa jijini Nairobi kati ya Julai 12 na Julai 16, 2017.
Ufichuzi huo wa malipo yasiyothibitishwa unajiri wakati Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) inajitahidi kukusanya mapato kufadhili miradi muhimu ya serikali.
Kulingana na ripoti ya KRA, ushuru uliokusanywa mwaka jana ulikosa kufikia kiwango kilicholengwa kwa zaidi ya Sh 84 bilioni.
Katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu Edward Ouko iliyowasilishwa bungeni na Kiongozi wa wengi kwenye bunge la kitaifa Aden Duale, idara ya serikali ya michezo ilitengewa Sh1.7 bilioni, michezo Sh 1.1 bilioni na Chuo Kikuu cha Kenyatta Sh 689.6milioni na kamati iliyohusisha wadau wote waliohusika na mashindano hayo iliyoundwa na wizara ili kusimamia matumizi ya fedha hizo.
Hata hivyo, Bw Ouko amezua maswali kuhusu matumizi ya pesa hizo kutokana na kutofuatwa kwa kanuni katika utoaji zabuni, matumizi ya hela ambayo hayajathibitishwa kutokana na ukosefu wa stakabadhi hitajika na deni linalodaiwa lilisalia la Sh 138.2 milioni.
Kamati ya uhasibu bungeni (PSC) inayoongozwa na Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi inatarajiwa kuangazia ripoti hiyo huku Sh349.6 milioni zikisemekana kutolewa bila kanuni za utoaji tenda kuzingatiwa, jambo ambalo ni kinyume cha kifungu cha sheria cha mwaka wa 2015 kuhusu utoaji tenda.
Katika ufichuzi huo, Sh66milioni zilitengewa zabuni ya huduma za uchukuzi wa teksi ambazo zilitolewa na kampuni ya Pewa Cabs Limited iliyolipwa Sh 23.8 milioni.
“Kampuni iyo hiyo ilipata kandarasi nyingine ya kutoa huduma za usafi na dobi kwa Sh 30.8miloni chini ya kamati andalizi ya mashindano hayo iliyoundwa,” akasema Bw Ouko katika ripoti.
Vile vile, zaidi ya Sh204.1 milioni zilitumika bila uwepo wa stakabadhi kuonyesha matumizi ya pesa hizo wala hakuna matangazo ya kibiashara yaliyochapisha kampuni zilizopata zabuni za kutoa huduma zilizotajwa inavyotakikana kisheria.
Kampuni za M/S Bonifide Group, Toyota Kenya Limited, Safaricom, M/S Harleys Limited na nyinginezo zilizodaiwa kutoa huduma zilipokea Sh94.6 miloni kwa jumla bila ushahidi wala thibitisho kwamba huduma hizo ziliafiki kiwango hicho cha fedha.
Swali jingine lililoibuliwa ni kutokamilishwa kwa ukarabati wa hoteli ya Sh 185.2 milioni, zabuni ambayo ilipewa kampuni ya M/S Protetta Holdings Limited ambayo haijamaliza kazi hiyo hadi leo.
Wakati huo huo, ripoti tofauti ya Bw Ouko ilionyesha kuwa idara ya maji iliyo chini ya Wizara ya Mazingira ilitumia Sh10.8 milioni kununua muda wa mawasiliano ya simu.
Mbali na kiwango hicho, ilibainika pia kwamba, idara hiyo ilitumia Sh5.2 milioni na Sh2.6 milioni kwa huduma za usalama na usafishaji ambazo kandarasi zilipeanwa kwa mashirika ya kibinafsi.
Katibu wa Wizara ya Maji, Bw Joseph Irungu, alisema huduma hizo zililipiwa licha ya kuwa kandarasi zilipitwa na muda mnamo Juni 30, 2013, hatua ambayo ni kinyume cha sheria.