Uhuru ‘amejenga’ walioshindwa
Na NICHOLAS KOMU
RAIS Uhuru Kenyatta amewatuliza wanasiasa waliopoteza nyadhifa zao katika ukanda wa Mlima Kenya kwenye uteuzi wa Chama cha Jubilee (JP) mnamo 2017 kwa kuwateua kuhudumu katika mashirika mbalimbali serikalini.
Wanasiasa hao hawakutetea nyadhifa zao hata baada ya kushindwa kwenye mchujo wa chama cha Jubilee.
Wengi kati ya wanasiasa hao wanatoka katika kaunti za Nyeri, Kiambu na Murang’a.
Wanasiasa saba kati ya wanane waliopoteza nyadhifa zao katika Kaunti ya Nyeri wameteuliwa kuhudumu kwenye mashirika hayo.
Ni aliyekuwa mbunge wa Tetu, Bw Ndung’u Gethenji pekee ambaye hajateuliwa.
Wale ambao wameteuliwa ni aliyekuwa mbunge wa Othaya Bi Mary Wambui kama mwenyekiti wa Mamlaka ya Kitaifa Kuhusu Ajira (NEA), aliyekuwa Seneta wa Nyeri, Bw Mutahi Kagwe kama mwanachama wa Bodi ya Kusimamia Kawi na Mafuta (EPRA) na aliyekuwa mbunge wa Mathira, Bw Peter Weru kama mwenyekiti wa Halmashauri ya Kusimamia Ustawishaji Mto Tana (TWWDA).
Uteuzi wao ulifuatia tangazo kwenye gazeti maalum la serikali mnamo Alhamisi.
Bw Kagwe aliteuliwa katika nafasi hiyo baada ya Waziri wa Kawi Charles Keter kufutilia mbali uteuzi wa Dkt Macharia Irungu.
Bw Kagwe aliibuka wa tatu kwenye kinyang’anyiro cha ugavana baada ya kushindwa na marehemu Gavana Wahome Gakuru.
Kwa upande wake, Bw Weru alimshukuru Rais Kenyatta kwa uteuzi huo, akiutaja kuwa “heshima kuu kwake na wakazi wa Mathira.”
Alihudumu kama mbunge kwa kipindi kimoja kati ya 2013 na 2017.