Uhuru atia saini Mswada wa Ugavi wa Fedha
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano ametia saini Mswada wa Ugavi wa Fedha baina ya Serikali za Kaunti (County Allocation of Revenue Bill-CARAB), 2019.
Mswada huo hutoa mwongozo na kiwango cha fedha ambazo kila serikali ya kaunti hupokea kutokana na mgao wa fedha zilizotengewa kaunti katika mwaka fulani wa matumizi ya fedha za serikali.
Unawezesha kutolewa kwa pesa hizo kutoka kwa Hazina ya Kitaifa hadi katika akaunti za benki za kila moja ya serikali 47 za kaunti. Katika mwaka huu wa serikali za kaunti zitapokea jumla ya Sh316.5 bilioni kama mgao wa kiusawa (equitable) na Sh61.1 bilioni kama mgao wa matumizi maalum kwa shughuli au miradi mahsusi (conditional grants/allocations).
Rais Kenyatta ameutia saini mswada huu saa chache baada ya kupitishwa na Bunge la Kitaifa na siku moja baada ya kupitishwa na bunge la seneti ambalo linaendesha vikao vyake katika kaunti ya Kitui.
Hatua hii pia inajiri siku moja baada ya Rais Kenyatta kutia saini Mswada wa Ugavi wa Fedha (DoRB) wa 2019 ambao unabaini mgao wa fedha kati ya Serikali Kuu na zile za kaunti. Hii ni baada ya wabunge na maseneta kuvutana kuhusu kiasi cha fedha zinazopasa kutengewa serikali za kaunti, mvutano uliodumu kwa miezi miwili.
Kutiwa kwa mswada wa CARB sasa kunamaanisha kuwa serikali za kaunti zitaanza kupokea Sh50 bilioni ambazo zilitolewa na Hazina ya Kitaifa Jumanne asubuhi kama mgao wa miezi ya Julai na Agosti.
Rais Kenyatta pia alitia saini mswada wa marekebisho ya sheria ya hatimiliki (Copyright Amendment Bill) 2019 .
Mswada huo unalenga kunyoosha mchakato wa ukusanyaji na ulipaji malipo kwa wasanii wa muziki na tungo nyingineza za sanaa.
Sherehe hiyo fupi ilihudhuria na Naibu Rais William Ruto, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Ken Lusaka. Wengine walikuwa ni kiongozi wa wengine katika bunge la kitaifa Aden Duale, Mkuu wa Sheria Paul Kihara na Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua.
Wengine walikuwa ni Naibu kiongozi wa wengi katika seneti Fatuma Dullo, Karani wa Bunge la Kitaifa Michael Sialai na mwenzake wa Seneti Jeremiah Nyegenye.