Uhuru awafuta kazi wanachama wote wa bodi ya shirika la feri
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta amewafuta kazi wanachama wote wa bodi ya Shirika la Feri Nchini (KFS), majuma matatu baada ya mkasa wa Likoni ambapo mwanamke na bintiye walikufa maji.
Katika notisi kwenye gazeti rasmi la serikali toleo la Oktoba 17, 2019, Rais Kenyatta amefutilia mbali uteuzi wa wanachama wote wa bodi hiyo.
“Kwa kuzingatia mamlaka kutokana na sehemu ya 7 (3) ya sheria za mashirika ya serikali, mie Uhuru Kenyatta, amirijeshi mkuu wa majeshi yote ya Jamhuri ya Kenya, nafutilia mbali uteuzi wa Dan Mwazo, Daula Omar, Naima Amir, Philip Ndolo, Rosina Nasigha Mruttu, kama mwenyekiti na wanachama wa bodi ya Shirika la Feri Nchini, kuanzia Oktoba 16, 2019,” notisi hiyo imesema.
Hatua hiyo inajiri baada ya Bi Mariam Kighenda na bintiye Amanda Mutheu kuzama mnamo Septemba 29, 2019, kisha kufariki baada ya gari lao kuteleza katika feri na MV Harambee katika kivuko cha Likoni na kutumbukia katika Bahari Hindi.
Miili yao ilipatikana baada ya shughuli ya uopoaji iliyoendeshwa kwa siku 13 kufuatia kazi ngumu iliyotelekezwa na wapigambizi kutoka Kikosi cha Jeshi la Wanamaji (Kenya Navy) na asasi nyingine.
Lakini ni baada ya kuwasili kwa wapigambizi kutoka Afrika Kusini ambapo gari hili liliweza kuopolewa kutoka baharini.
Inatarajiwa kwamba miili ya wawili hao itazikwa Jumamosi nyumbani kwa mumewe marehemu Kighenda, John Wambua, katika Kaunti ya Makueni.