Uhuru awaomba malandilodi kuwa na utu
Na SAMMY WAWERU
Rais Uhuru Kenyatta amewataka wamiliki wa majumba ya kupangisha maarufu kama malandilodi kuwa na utu wakati huu Wakenya wanapitia nyakati ngumu kufuatia athari za Covid – 19.
Kwenye mahojiano ya pamoja mnamo Jumatano na vituo vya redio vinavyopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili, kiongozi wa nchi alisema huu ndio wakati ambao malandilodi wanapaswa kuonyesha ubinadamu kwa wapangaji.
“Tumefunzwa kuwa na utu, ninawasihi malandilodi kuonyesha utu kwa wapangaji wao,” Rais Kenyatta akasema, akieleza hisia zake kufuatia matukio ya baadhi ya malandilodi kufurusha wapangaji kwa kushindwa kulipa kodi ya nyumba.
Visa kadhaa vya wapangaji kufukuzwa usiku na mapaa ya nyumba wanazoishi kung’olewa vimeripotiwa maeneo mbalimbali nchini, kwa kinachotajwa kama kushindwa kulipa kodi. Hata hivyo, kuna wachache waliopunguzia wapangaji kodi na kadhaa kusitisha ulipaji kwa muda.
Tangu kisa cha kwanza cha virusi vya corona kutangazwa nchini, sekta ya biashara na ambayo imeajiri idadi kuu ya Wakenya imeathirika pakubwa na uchumi kuzorota. Baadhi ya biashara na hata kampuni zimefungwa kwa kushindwa kuhudumu katika mazingira magumu yanayosababishwa na Covid – 19.
Isitoshe, wafanyakazi wamesimamishwa kazi na kampuni na mashirika yanayoendelea kuhudumu wafanyakazi kadhaa wakipewa likizo ya lazima. Pia, taasisi mbalimbali za serikali na kampuni za kibinafsi zimetangaza kupunguza mishahara ya wafanyakazi.
a“Hili ni janga la kimataifa, limeathiri kila kona ya ulimwengu. Biashara na uchumi zimeathirika na ni ishara watu wanapitia magumu,” Rais akasisitiza kwenye mahojiano hayo. Vituo vilivyopeperusha mahojiano hayo moja kwa moja kutoka Ikulu, Nairobi, vinajumuisha Redio Citizen, Redio Jambo, Milele Fm na KBC Redio Taifa.