Habari MsetoSiasa

Uhuru awarai wawekezaji Amerika wamsaidie kuafikia Ajenda Nne Kuu

August 28th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

RAIS Uhuru Kenyatta amepigia debe Kenya katika ziara yake nchini Marekani, akiwahimiza wawekezaji wa taifa hilo kuja humu nchini kuwekeza zaidi ili kumsaidia kutimiza ndoto yake ya Ajenda Nne Kuu.

Katika mikutano ya kibiashara na baadhi ya kampuni kubwa za Marekani Jumatatu, Rais aliwahimiza wawekezaji kuzingatia malengo yake manne makuu anayonuia kutimiza katika kipindi chake cha mwisho na kuyatumia kama nafasi ya kuwekeza humu nchini.

Rais Kenyatta alitoa hakikisho kwamba serikali yake imejitolea kuondoa vikwazo vinavyoweza kuzuia wawekezaji kutoka nje kufanya biashara Kenya, ili maendeleo yatimie.

“Kenya iko tayari kwa biashara na tungependa kuimarisha ushirikiano huu kwa manufaa ya sekta ya kibinafsi na Wakenya. Katika kipindi changu cha pili, nimepea kipau mbele masuala manne ya kuleta maendeleo na kubuni ajira, hizo ni nafasi za kuwekeza,” Rais Kenyatta akasema.

Wakati wa mikutano hiyo, Rais Kenyatta alishuhudia kutiwa saini kwa mikataba miwili ya kibiashara ambayo itawezesha makampuni mawili ya Marekani kuwekeza kwenye miradi inayogharimu jumla ya zaidi ya Sh23bilioni katika sekta ya umeme, kwenye ufadhili utakaozalisha megawati 100 kutumiwa kusini mwa Nairobi.

Rais aidha alisema kuwa Kenya inapania kuongeza kiwango cha utengenezaji bidhaa kutoka asilimia 8.4 hadi 15 kufikia 2022.

“Hatua hii inatoa fursa kwa waekezaji wa kimataifa na wa Kenya katika nyanja za kuanzisha viwanda vya kuongezea thamani bidhaa za kilimo, utengenezaji bidhaa za nguo na ngozi, na nyingine,” akasema Rais.

Aidha, kenya ilipata afueni kwenye sekta ya chakula, kupitia hatua ya kampuni ya Twiga foods kuekeza dola milioni tano katika sekta ya kilimo.

Rais Kenyatta alipongeza kampuni hiyo, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza chakula humu nchini haswa kwa kuinua kilimo.

Rais Kenyatta alisifu Kenya kuwa imeboresha mazingira ya biashara, kiwango cha kutambuliwa bara Afrika na ulimwenguni.

“Kati ya 2014 na 2018, Kenya imeimarisha ubora wake wa kibiashara kulingana na Benki ya Dunia, iliyoorodhesha kenya kuwa nambari 80 kwa mazingira bora ya kibiashara, kutoka nambari 136,” akasema Rais Kenyatta.

Aliongeza kuwa mwaka huu Kenya inashikilia nafasi ya nane kama taifa bora la kibiashara barani Afrika kutoka nambari 15 mwaka jana.