Habari MsetoSiasa

Uhusiano wangu na Moi ulikuwa kama wa baba na mwana – Lee Njiru

February 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na STELLA CHERONO

MSAIDIZI wa kibinafsi wa Rais Mstaafu Daniel arap Moi aliye pia Katibu wake wa Habari, Bw Lee Njiru huaminika kufahamu siri zake za ndani.

Kufikia wakati Mzee Moi alipofariki Jumanne alfajiri, Bw Njiru alikuwa mwandani wake mkubwa.

Katika mahojiano na Taifa Leo Jumatano, Bw Njiru ambaye alimhudumia Mzee Moi kwa miaka 43 alifichua jinsi uhusiano wao ulivyokuwa.

“Bw Moi alikuwa kama babangu,” alisema.

Wakati aliyekuwa rais Mwai Kibaki alipoingia mamlakani baada ya Mzee Moi, Bw Njiru aliendelea kumfanyia kazi rais huyo mstaafu ambaye aligeuka kuwa ‘mpweke na mkimya’, akiishi katika nyumba zake za Kabarak iliyo Nakuru na Kabarnet Gardens jijini Nairobi.

“Uhusiano wetu ulibadilika kutoka kuwa wa mwajiri na mwajiriwa wake, hadi kuwa kama wa baba na mwanawe. Alinifunza. Alikuwa mtu mkarimu zaidi na mwaminifu ambaye nimewahi kukutana naye maishani mwangu. Aliamini kuhusu bidii,” akasema Bw Njiru wakati wa mahojiano katika hoteli yake ya Cherrynam Resort iliyo Nakuru.

Afisa huyo wa mawasiliano ambaye anasisitiza hajastaafu kutoka kwa wadhifa wake, alisema Mzee Moi alimtetea hata wakati ‘mahasimu’ walipojaribu kumpiga vita.

Bw Njiru, ambaye alizaliwa Runyenjes katika mwaka wa 1949, alisoma katika Shule ya Upili ya Kangaru hadi mwaka wa 1968 kisha akajiunga na taasisi ya Kenya Institute of Mass Communications katika mwaka wa 1974.

Alipata diploma ya uanahabari kisha katika mwaka wa 1975, akapelekwa kufanya kazi Kakamega kama afisa wa habari wakati wa utawala wa hayati Mzee Jomo Kenyatta.

“Wakati huo marehemu Moi alikuwa ni Makamu wa Rais aliyekuwa mwaminifu sana kwa rais,” akasema.

Baadaye alihamishwa kutoka Kakamega hadi Nairobi kuchukua mahali pa Francis Mungai Kamau.

Alikuwa na umri wa miaka 28 pekee wakati alipoanza kufanya kazi katika Ikulu kama afisa katika idara ya habari na mawasiliano ya rais, mwaka wa 1976.

Mkutano wa kwanza aliowahi kuhudhuria ulikuwa katika Ikulu ya Nakuru ambapo ndipo alifaa kufanyia kazi.

Alikutana na aliyekuwa waziri mwenye ushawishi mkubwa Mbiyu Koinange ambaye alimwarifu kabla Mzee Kenyatta kujiunga nao baadaye.

“Kenyatta aliniuliza kama nilikuwa tayari kufanya kazi zake, nikamjibu ‘nitajaribu’. Alikasirika sana akaniambia ‘kazi yangu hutekelezwa, haijaribiwi’,” akaeleza.

Bw Njiru alisema wakati alipojiunga na idara ya habari ya rais, afya ya Mzee Kenyatta ilikuwa imeanza kudorora na hivyo basi Mzee Moi ndiye alifanya majukumu mengi ya urais ikiwemo kuhudhuria hafla za kimataifa.

Mzee Kenyatta alipofariki mwaka wa 1978, Bw Njiru ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 30 aliendelea kufanya kazi katika Ikulu hadi Mzee Moi akaingia mamlakani.

Ziara yake ya kwanza na Mzee Moi ilikuwa London, Uingereza katika mwaka wa 1981. Katika ziara hiyo ambayo anasema ilikuwa ya muda mrefu zaidi kwao pamoja, walienda pia Washington, Honolulu, Australia, Kuala Lumpur, Karachi na mataifa mengine kwa siku 21.

Kadri na jinsi muda ulivyosonga, Bw Njiru alipata umaarufu kama afisa mwenye ushawishi mkubwa wa Moi ambaye ni mwenye asili ya nje ya Rift Valley.

Hali hii ilimfanya kuchukiwa na viongozi wa Rift Valley waliotaka atimuliwe, lakini anasema Mzee Moi alimtetea akakataa ukabila.