Ujenzi wa barabara ya Dongo Kundu waanza
Na MOHAMED AHMED
WAJENZI wa sehemu ya pili na ya tatu ya barabara ya Dongo Kundu inayogharimu mabilioni ya pesa wapo tayari kuanza ujenzi huo.
Hii ni baada ya Halmashauri ya barabara kuu za Kitaifa (KeNHA) kutia sahihi mkataba wa ujenzi huo.
“Wajenzi tayari wamefika na muda wowote kuanzia sasa ujenzi ramsi utaanza, vile vile tumeweza kutia sahihi kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya pili. Barabara zote hizo zinapaswa kuanza,” akasema afisa wa mawasiliano ya KeNHA Charles Njogu.
Alisema kuwa wajenzi hao tayari wameanza kukusanya vifaa husika kwa ajili ya shughuli hiyo inayotazamiwa kuchukua miaka miwili.
Sehemu hiyo ya pili ya barabara hiyo itahusisha barabara ya kilomita 8.9 kati ya eneo la Mwache na Mteza. Kisha kutakuwa na ujenzi wa madaraja katika kijiji cha Mwache na daraja lengine katika kijiji cha Mteza.
Kampuni ya Japanese Consortium Fujita Corporation/Mitsubishi Corporation imepewa nafasi ya ujenzi huo wa sehemu ya pili itakayogharimu Sh24 bilioni.
Sehemu ya tatu ya barabara hiyo itakuwa ile ya kilomita 6.9 ambayo itajengwa baina ya Mteza na Kibundani, na kuanganisha barabara kuu ya Likoni-Lunga Lunga.
Barabara ya Dongo Kundu, sehemu ya kwanza ambayo ilijengwa kwa thamani ya Sh11 bilioni ilifunguliwa rasmi mwezi Juni mwaka jana.
Ujenzi wa barabara hiyo ulianzia katika eneo la pili la egesho la bandari ya Mombasa hadi eneo la Bonje karibu na mji wa Mazeras. Ujenzi wake ulianza mwaka 2016.
Mpango wa ujenzi wa barabara hii ulitolewa miaka 30 iliyopita na ulipangwa kutatua shida ya msongamano wa magari unaokumba kisiwa cha Mombasa.
Ujenzi wa Dongo Kundu tayari umeanza kuonekana kuwa na manufaa kwa wakazi wa Pwani.
Utakapokamilika, itakuwa rahisi kwa watalii kufika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi, bila kulazimika kwa mfano, kutumia feri kutoka Pwani Kusini.
Wadau katika sekta ya Utalii katika kaunti ya Kwale, wamekuwa wakilalama dhidi ya kucheleweshwa watalii kwenye kivuko cha feri cha Likoni.