Ukarabati wa barabara ya Riat-Ndhiwa kuwafaa wafanyabiashara Homa Bay
Na VALENTINE OBARA
JAMII na wafanyabiashara katika eneo la Ndhiwa, Kaunti ya Homa Bay wanatarajia kunufaika pakubwa na ukarabati wa barabara ya Riat-Ndhiwa.
Barabara hiyo ya umbali wa kilomita 10 ambayo imekuwa katika hali mbovu kwa miaka mingi inafanyiwa ukarabati kwa udhamini wa kampuni ya Sukari Industries.
Mhandisi Mkuu wa kampuni hiyo, Bw Boaz Amoke, alisema ukarabati mzima utagharimu Sh12 milioni na unafanywa kwa njia ya kuwezesha ubora wa kudumu kwa miaka miwili kabla ukarabati mwingine kuhitajika.
Wakazi waliohojiwa walisema kando na kutatiza usafiri ikiwemo wa dharura kama vile kuenda hospitalini, hali mbaya ya barabara ilikuwa pia ikiwaletea vumbi jingi kwa kiasi cha kuathiri afya yao.
Meneja Mkuu wa Sukari Industries, Bw David Okoth alifichua kwamba shughuli za kampuni pia zilikuwa zikiathirika kwa hali mbaya ya barabara.
“Trekta zetu na malori yalikuwa yakikwama barabarani na kuchelewesha sana shughuli kiwandani,” akaeleza Bw Okoth.
Alitoa wito kwa serikali ya kaunti na serikali kuu kuchangia ili barabara itiwe lami baadaye kwa manufaa ya wakazi.
Kauli hii iliungwa mkono na wakazi ambao wanaamini hali mbaya ya barabara huchangia katika gharama kubwa ya maisha.
“Wakitia lami kwa hii barabara itachukua dakika tano tu kusafiri kutoka mjini Ndhiwa hadi Riat. Gharama ya usafiri itashuka, kumaanisha biashara pia zitafaidika,” akasema mwenyekiti wa wahudumu wa boda boda katika Kaunti Ndogo ya Ndhiwa, Bw Dan Nyakwana.
Idadi kubwa ya vibarua walioajiriwa kufanya ukarabati ni wa jamii zinazopakana na barabara hiyo.
Kampuni ya Sukari Industries ambayo hutengeneza sukari ya Ndhiwa Sugar, imefanyia ukarabati barabara nyingine kadhaa katika eneo hilo.