Habari Mseto

Ukatili wanaofanyiwa mabinti wakikeketwa

November 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA PHYLIS MUSASIA

MADAKTARI kutoka Hospitali ya Nakuru jana walishangaa walipopata matone ya mafuta taa na mkojo kwenye chembechembe za damu za wahasiriwa wawili wa ukeketaji baada ya kufanyiwa uchunguzi kwenye maabara ya hospitali hiyo.

Wasichana hao wawili wenye umri wa miaka 15 na 13 kutoka kijiji kimoja eneo la Elementaita, Kaunti ndogo ya Naivasha, walifichua kwamba mkeketaji aliwapaka mafuta taa kisha kuwaambia wawe wakijipaka mkojo ili kidonda kipoe haraka.

Muuguzi Teophila Murage alifichua kwamba wasichana hao walikeketwa vibaya kiasi kwamba maisha yao yalikuwa hatarini.

Waliokolewa na polisi wakiwa na majeraha mabaya.Kulingana na taarifa waliyoandika, wahasiriwa hao walidai kwamba walikeketwa baada ya kusafiri hadi kwa makazi ya mama yao shule zilipofungwa kutokana na amri ya baba yao.

“Tumeishi na baba yetu kwa muda mrefu baada yake kutengana na mama. Tuliwasili salama salmini kwa makazi ya mama lakini tukakeketwa siku chache baadaye,” ikasema taarifa yao.

Walifafanua kwamba mwanamke wasiyemfahamu aliwasili akiwa ameandamana na baba yao saa tano usiku na mwanamke huyo akawakeketa huku baba yao akiatazama tu.

Polisi kutoka kituo cha polisi cha Elementaita alisema baba ya mabinti hao aliandikisha taarifa akidai kwamba aliyekuwa mkewe alikuwa amewafadhili ngariba aliyewakeketa wasichana hao.

Mama ya watoto hao ambaye anaendelea kuzuiliwa katika kituo hicho cha polisi, naye aliwaeleza polisi kwamba ni baba ya watoto hao ndiye alipanga ukeketaji wa wasichana hao wala si yeye.