• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Ukiachwa achika, usiue mtu sababu ya mapenzi – Gavana Nassir

Ukiachwa achika, usiue mtu sababu ya mapenzi – Gavana Nassir

WINNIE ATIENO NA KNA

GAVANA wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, amewashauri vijana kukubali wanapokataliwa na wanawake badala ya kuua kwa sababu ya mapenzi.

Akiongea katika hafla ya kupinga mauaji ya wanawake iliyoandaliwa Mombasa mnamo Jumatano, Bw Nassir alisema nguvu za mtu hubainishwa na jinsi anavyoweza kujidhibiti.

“Mtu mwenye nguvu hasababishi vita bali hudhibiti moyo wake ili asimdhuru mtu yeyote,” akasema.

Hafla hiyo ilikuwa imeandaliwa na wanaharakati katika kituo cha Swahili Pot mjini Mombasa kwa kumbukumbu ya wanawake waliouawa na wapendwa wao.

Bi Joyce Achieng, mwandalizi wa hafla, alisema lengo kuu ni kukumbuka maisha ya wanawake ambao wameuawa na wapenzi wao au watu wasiowajua.

“Leo ni siku ya wapendanao, siku inayojulikana kwa wapendanao na wanawake hawa ambao wameuawa hawakufanikiwa leo kutumia wakati na wapenzi wao,” akasema Bi Achieng.

Ajra Mohamed, mwanachama wa vuguvugu la End Femicide KE alisema hafla hiyo ni njia ya kuonyesha upendo kwa wanawake waliopoteza maisha kwa kuuawa.

“Tunataka pia kuonyesha upendo wetu kwa haki na nchi. Tunataka nchi iwe salama zaidi kwa wanawake kutoishi kwa hofu ya kushambuliwa au kufanyiwa Ukatili wa Kijinsia (GBV). Mauaji ya wanawake ni mojawapo ya aina za GBV uliokithiri,” alisema Mohamed.

Wanaharakati hao wanataka mapendekezo yaliyowasilishwa kwa Serikali ya Kitaifa na Kaunti kutekelezwa.

Baadhi ya mapendekezo hayo ni kwa Idara ya Mahakama kuharakisha kesi za mauaji ya wanawake na kuanzishwa kwa vituo vya Unyanyasaji wa Kijinsia katika kaunti.

Kwingineko, Gavana Nassir, amewasihi wakazi kujitolea kutoa damu ya kusaidia wagonjwa hospitalini.

Akiongea katika bustani ya Treasury Square, Bw Nassir alisema hospitali zinakumbwa na uhaba wa damu.

Akiongea katika zoezi la utoaji damu, Bw Nassir alisema alijitokeza kutoa damu ili kuwatia moyo wakazi wa Mombasa kujitokeza kwa wingi kusaidia wengine.

  • Tags

You can share this post!

Kocha Gervais Hakizimana: Kielelezo cha urafiki wa kufa...

Mjukuu wa Moi ataka familia ifanyiwe DNA

T L