Ukurasa wa Seneta Nyutu wadukuliwa saa chache baada ya kuunga Ndindi Nyoro kwa urais 2032
Na MWANGI MUIRURI
Baadhi ya wanasiasa katika eneo la Kati sasa wamehusisha kudukuliwa kwa mitandao kadha yao ya Facebook na harakati zao za kumpigia debe mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro kuwania urais 2032.
Katika siku za hivi punde, mtandao wa Bw Nyoro ulidukuliwa na picha za aibu zikapachikwa huku nao ule wa Seneta wa Murang’a, Joe Nyutu ukitekwa nyara Alhamisi punde tu baada ya kutangaza alikuwa akiunga mkono mbunge huyo wa Kiharu kuwa kinara wa siasa za Mlima Kenya.
Huku kukiwa na uhasama fiche kati ya Nyoro na Naibu wa Rais Rigathi Gachagua katika uthibiti wa siasa za eneo hilo la Mlima, wenyeji wanafuatilia kuona hali itakavyoendelea kuzua mtitimuano ambao bila shaka unazidi kusukwa kichinichini.
Mnamo Ijumaa, Bw Nyutu aliteta kwamba “huku Mlima Kenya tuko na baadhi ya wanasiasa ambao hawana mbinu ya kuchumbia wafuasi lakini wamekuwa wakitumia mabavu na cheo chao cha juu kutushinikiza kumfuata kama kinara wetu”.
Bw Nyutu alisema kwamba “hizi njama zote unazoziona zikitekelezewa baadhi yetu ni za kuadhibu wanaoonekana wakaidi kwa ufuasi wa mtu fulani na kujaribu kutuonyesha kana kwamba hatuna bongo huru za kujifanyia maamuzi”.
Jioni hiyo nao ukurasa wake wa Facebook ukadukuliwa na ukaanza kutumiwa kutuma jumbe za ombaomba na utapeli pamoja na filamu za aibu.
Bw Nyoro alisema kwamba “hii ni kazi ya wasio na la kufanya na bila shaka watashindwa”.
Bw Nyutu aliteta kwamba baada ya wadukuzi hao kuteka nyara mitandao hiyo “waliweka jumbe za kutuangazia kama wachafu kimaadili na mimi hasa nikiangaziwa kama ombaomba na tapeli aliyekuwa akiwaelekeza wafuasi wanitumie Sh10 ndio nami niwatumie Sh2, 000 kama zawadi.
Mbunge wa Gatundu Kaskazini Bw Elijah Kururia ambaye pia alitangaza Alhamisi kwamba “hakuna kiongozi Mlima Kenya isipokuwa Nyoro” alisema mitandao yake ilikuwa ikijaribiwa katika njama za udukuzi.
“Mimi sitabadili msimamo wangu kwamba katika eneo la Mlima Kenya hakuna mwanasiasa anayempiku Bw Nyoro katika harakati za kuunganisha. Hakuna na ndiyo sababu tunamzingatia awanie urais 2032 baada ya Rais William Ruto kustaafu,” akasema.
Wanasiasa wengine ambao wameteta kuhusu njama hizo ni pamoja na mbunge wa Githunguri Bi Gathoni wa Muchomba na pia aliyekuwa kinara wa kundi haramu la Mungiki Bw Maina Njenga.
“Hata kuzuke njama gani mimi sitakoma kumtetea mwananchi wa kawaida katika masuala ya kiutawala. Wamejaribu njama nyingi lakini hatimaye kandarasi yangu iko kati yangu na wapiga kura wangu,” akasema wa Muchomba.
Bw Njenga alisema “hawa waoga hawahusiki tu na njama za kudunisha wengine…hata wanatishia wengine maisha huku wakiwabandika majina ya aibu ndio wapate fursa ya kukandamiza kwa nguvu za vyeo vyao”.
Alisema “njama zote chafu na mikakati ya kudunishana ni himaya ya mrengo mmoja tu wa kisiasa na mnajua unaongozwa na nani kwa kuwa yeye huongea hadharani kila mtu akishuhudia”.
Hata hivyo, alisema kwamba “hawatuwezi”.