Habari Mseto

Ukweli kuhusu kufungwa kwa Chase Bank wafichuliwa

May 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYAKAZI wa ngazi za juu katika benki ya National (NBK) Jumatatu alieleza sababu za kufungwa kwa benki ya Chase Bank miaka mitatu iliyopita.

Bw Eustace Kariuki Nyaga alimweleza hakimu mwandamizi Martha Mutuku ripoti ya uhasibu ya Benki Kuu ya Kenya (CBK) na kampuni ya Uhasibu ya Delloite kuhusu benki hiyo ilipelekea benki ya Chase kufunga milango.

Bw Nyaga alieleza korti inayosikiza kesi ya Sh1.6bn dhidi ya aliyekuwa mwenyekiti Mohammed Zafrullah Khan na wengine tisa kuwa ripoti ya uhasibu ya CBK na Delloite iliwafanya wateja wake kupata mshtuko kisha wakakimbia kutoa pesa zao.

“Wateja waliposoma ripoti iliyochapishwa na CBK na Delloite katika vyomba vya habari na katika mitandao ya kijamii, wateja walikimbia kutoa pesa na kuipelekea kufungwa,” alisema Bw Nyaga.

Mwanabenki huyo aliyejiunga na Chase Bank 2014 alisema kazi yake ilikuwa kusimamia kitengo cha mikopo.

“Nilikuwa nasimamia kitengo cha mikopo na ningelisoma pesa zote zilizokuwa zimetolewa kwa wateja,” alisema Bw Nyaga.

Mfanyakazi wa NBK Eustace Kariuki Nyaga. Picha/ Richard Munguti

Akihojiwa na wakili David Chege kutoka kwa kampuni ya Mawakili ya Cecil Miller , Bw Nyaga alisema “hakuna benki isiyo na kasoro katika utenda kazi wake na hakuna benki inayoweza kuwazuia wateja wake kutoa pesa zao zote na kufunga akaunti zake.”

Washukiwa hao wanadaiwa walipora benki hiyo zaidi ya Sh1.6bn.

Akiongozwa kutoa ushahidi na Bi Rubby Okoth , Bw Nyaga alisema kabla ya kujiunga na Chase Bank alikuwa amehudumu katika benki ya Barclays kwa muda wa miaka 16.

“ Uko na uzoefu mkubwa katika utenda kazi katika benki,” wakili Chege alimwuliza shahidi huyo.

Mahakama ilielezwa ripoti ya CBK ya uhasibu ya Machi 2016 ndiyo ilisababisha wateja kuondoa pesa kwa pupa hata viwango vikashuka na kupelekea benki kuu kuifunga mara moja.

Sasa benki hiyo iliwekwa chini ya usimamizi wa Kenya Commercial Bank (KCB).

Shahidi huyo wa kwanza kutoa ushahidi dhidi ya Bw Khan alisema “siwezi kuzugumzia hali ya fedha ya Chase Bank kabla ya 2009.”

Alikuwa akitoa ushahidi dhidi ya Bw Khan anayeshtakiwa pamoja na Mabw Duncan Kabui Gichui , James Mwaura na Makarious Omondi Agumbi,Wengine ni Amira Claudia Wagner, Mohammed Najifrullah Khan na kampuni za Camellia Investments Limited, Colnbrook Holdings Ltd, Golden Azure Investments na Cleopatra Holdings Ltd.

Bw Mohammed Zafrullah Khan (kulia) na washukiwa wengine wakiwa kizimbani. . Picha/RICHARD MUNGUTI

Kumi hawa wamekana kufanya nja za kuiba Sh529,328,000 na Dola za 1,326,000 (Sh132,600,000) ambapo makampuni ya Camellia,Colbrook,Golden Azure na Cleopatra kwa kudai kitita hicho kilikuwa kimetolewa kama mikopo.

Yadaiwa walitekeleza uhalifu huo kati ya Agosti 28 2008 na Machi 3 2016. Mabw Mwaura na Omondi wamekana kuiba Sh483,328.

Zafrullah, Kabui, Mwaura na Omondi wamekana kuiba Sh46m mnamo Februar1 28,2012.

Mashtaka mengine yasema mnamo Desemba 2015, Zafrullah, Mwaura, Omondi na kampuni ya Camellia waliiba Sh483,328,000 mali ya benki hiyo.

Zafrullah na kampuni ya Colnbrook waliiba Dola 108,000 mnami Februar1 28, 2012 nao Mwaura na Omondi walikana kuiba dola 588,000 mnamo Desemba 31, 2015.

Vile vile Zafrullah Kabui,Omondi, Mwaura na kampuni ya Cleopatra wamekana wizi wa Dola630,000 mnamo Februari 28, 2009.

Mabw Zafrullah, Omondi na Kabui wameshtakiwa kukataa kuripoti utoaji wa viwango vya pesa vilivyozidi Dola za marekani 10,000 kwa CBK.

Wakuu hao walishtakiwa kwa kukosa kuelezea makao makuu ya Chase kwamba Dola za Marekani 630,000 ,108,000 na Sh46m zilitolewa kwa njia ya utata.

Kesi inaendelea.