Habari Mseto

Ulegevu wa polisi unavyochochea ghasia za kisiasa Kisii

May 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RUTH MBULA

MAPUUZA ya polisi kutochukua hatua zozote za kuzima uhuni yanasemekana kuchangia uendelevu wa fujo za kisiasa zinazozidi kutokea katika Kaunti ya Kisii.

Licha ya hakikisho kutoka kwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki, kwamba wachochezi watazimwa, visa hivyo vingali vinatokea.

Katika hali ambapo polisi hujaribu kuwakamata washukiwa, wakuu wao huhamishiwa sehemu nyingine na wale waliohusika na machafuko hayo huachwa kupanga na kufanya vurugu zaidi.

Taifa Leo imebaini kuwa baadhi ya wanasiasa ndani ya Muungano wa Kenya Kwanza kutoka Kisii hushirikiana na watu wenye mamlaka ndani ya Wizara ya Usalama wa Ndani kuhujumu kazi huru ya polisi.

Katika kisa cha hivi punde cha fujo za kisiasa, wabunge kutoka kaunti hiyo na wafuasi wao walipigana bila aibu katika hafla ya kuchangisha pesa ya Kanisa la PAG huko Etono, eneobunge la Bomachoge Borabu siku ya Jumapili.

Kinara wa Wengi katika Bunge la Kitaifa na Mbunge wa Mugirango Kusini, Silvanus Osoro, alikuwa amealikwa kama mgeni mkuu.

Madai yaliibuka kuwa mbunge wa eneo hilo, Obadiah Barongo wa chama cha ODM, alikuwa ametengwa katika hafla hiyo lakini alihudhuria akiwa ameandamana na wafuasi wake.

Pia katika mchango huo, kulikuwa na madiwani kadhaa na wabunge Patrick Osero (Borabu), Joash Nyamoko (Mugirango Kaskazini), Japheth Nyakundi (Kitutu Chache Kaskazini) na Anthony Kibagendi (Kitutu Chache Kusini).

Bw Kibagendi, mshirika wa karibu wa Bw Barongo na mkosoaji mkali wa Rais William Ruto, alikashifu viongozi wa UDA kwa kutokuwa waaminifu kwa wananchi na kwa kuhamasisha walalahoi kuwazomea baadhi ya viongozi.

“Nilikuja hapa na Dkt Ruto na akaahidi kupunguza ushuru katika mfumo wake wa kuanzia chini kwenda juu (Bottom Up) lakini hayo hayajafanyika,” Bw Kibagendi alisema huku kukiwa na shangwe na vifijo.

Aliendelea: “Baadhi yenu mmelipwa ili kuzomea na kukashifu viongozi lakini nitakuja kwenu na kuwashughulikia mmoja mmoja.” Alipokuwa akiongea, vipaza sauti vilizimwa huku baadhi ya vijana wakisonga mbele na kuanza kumbana. Nyimbo za ODM na UDA zilitanda hewani.

Hali ilipotishia kuwa mbaya, polisi walirusha vitoa machozi na kuwalazimisha waumini kutorokea usalama wao.

Utulivu ulirejea baadaye Mbunge Osoro alipochukua maikrofoni na kuomba msamaha kwa yaliyojiri.

Bw Osoro, aliwataka wakazi kutopigana kwa sababu ya siasa, akisema wanasiasa si maadui.

Kufikia kuchapishwa kwa taarifa hii, hakuna yeyote aliyekamatwa kutokana na ghasia hizo licha ya video nyingi kuzagazwa mitandaoni zikionyesha vijana waliokuwa “wakimfinya” mbunge Kibagendi.

Mnamo Juni 6, 2023, kulitokea vurumai Mugirango Kusini katika ibada ya mazishi ya babake MCA wa Boikang’a.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na Bw Osoro na gavana Arati miongoni mwawaomboleza wengine. Ghasia zilizuka na kuwaacha waombolezaji wakihangaika kutafuta usalama wao. Polisi hawajamkamata mtu yeyote kwa machafuko hayo.

Mnamo Januari 8, 2024 gavana Arati na mbunge Osoro walizozana tena Nyakembene eneo bunge la Mugirango Kusini wakati wa hafla ya kujaza fomu za masomo iliyoongozwa na Bw Arati.

Watu wasiojulikana waliojihami kwa bunduki walifyatulia umma risasi na kuwasababishia majeraha mabaya.

Kesi hiyo iliripotiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Kisii lakini hakuna aliyekamatwa kufikia sasa.

Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki alizuru Kaunti ya Kisii na kuahidi kuhakikisha kuwa wahuni wa kisiasa wamekamatwa lakini maneno yake sasa yanaonekana kuwa matupu.

“Mtaona watu wakikamatwa katika wiki zijazo kwa wale wanaotaka kusababisha ghasia. Kama vyombo vya usalama tumejitolea kuhakikisha kuwa kila Mkenya yuko salama kwani hakuna aliye juu ya sheria,” alisema waziri katika gereza la Kisii.